AFRIKA KUSINI-SIASA-ANC-USHINDI-2019

Rais Ramaphosa awaongoza wafuasi wa ANC kusherehekea ushindi wa Uchaguzi Mkuu

Rais wa Afrika Kusini  Cyril Ramaphosa
Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa REUTERS/Mike Hutchings

Wafuasi wa chama tawala nchini Afrika Kusini cha  ANC wamekuwa wakisherehekea ushindi wa Uchaguzi Mkuu uliofanyika wiki hii, baada ya kutangazwa mshindi licha ya ushindani mkali.

Matangazo ya kibiashara

Chama cha ANC kilipata ushindi wa asilimia 57.5 kwa mujibu wa matokeo ya mwisho yaliyotangazwa na Tume ya Uchaguzi siku ya Jumamosi.

Nafasi ya pili ilichukuliwa na chama cha Democratic Alliance huku chama cha EFF kinachoongozwa na Julius Malema kikichukua nafasi ya tatu.

Rais Cyril Ramaphosa akiwaongoza wafuasi wa chama hicho, kusherehekea ushindi huo katika makao makuu ya chama hicho,  amesema wapinzani wameaibika .

"Tunasema, asante, asanteni sana kwa watu wa Afrika Kusini, kwa kurejesha vuguvugu pekee linaloweza kupeleka nchi yetu mbele, vuguvugu pekee la ANC,"  alisema huku akishangiliwa.

"Tunawaambia watu wetu kuwa tunawashukuru kwa unyeyekevu mkubwa na kuiamini ANC, uchaguzi huu ulikuwa ni mgumu, walifikiri ANC ingepoteza lakini, tumewaonesha kuwa, ANC ni vuguvugu lenye ushindi linaloaminiwa na watu wetu," aliongeza rais Ramaphosa.

Hata hivyo, chama cha ANC kinarejea madarakani kikiwa na wabunge wachache ikilinganishwa na uchaguzi uliopita huku rais Ramaphosa akikibaliwa na kazi kubwa ya kupambana na ufisadi, kuunda nafasi za ajira hasa kwa vijana miongoni mwa changamoto nyingine.