BURKINA FASO-MAUAJI-USALAMA

Mauaji Burkina Faso: Rais Kabore awataka raia wake kuwa waangalifu

Dablo inapatikana kilomita 90 kutoka Kaya.
Dablo inapatikana kilomita 90 kutoka Kaya. Google Map

Maafisa wa serikali nchini Burkina Faso wamethibitisha kuuawa kwa kuhani na wahudumu watano wakati wa ibada ya misa siku ya Jumapili katika shambulio lililolenga kanisa Katoliki jijini Dablo, kaskazini mwa Burkina Faso.

Matangazo ya kibiashara

Meya wa Mji wa Dablo Ousmane Zongo amesema mapema wakati wa misa watu wenye silaha walijitokeza Kanisani na kuanza kuvurumisha risase pale tu walipoona waumini wameanza kukimbia.

Washambuliaji hao wanakadiriwa kuwa kati ya 20 na 30 hivi waliwateka baadhi ya waumini na kuawauwa watano kati yao pamoja na Kuhani ambae alikuwa akiadhimisha misa na kisha wakateketeza kwa moto kanisa hilo pamoja na maduka kadhaa na kupora madawa kabla ya kuchoma moto gari la muuguzi mkuu katika eneo hilo.

Mashuhuda wanasema shambulio hilo lilidumu kwa muda wa saa moja.

Jeshi la serikali limeshindwa kuingilia kati shambulio hilo kutokana na kwamba washambuliaji hao walikuwa wengi kuliko idadi ya wanajeshi waliokuwepo katika eneo hilo, kwa mujibu wa Meya wa mji wa Dablo, Ousmane Zongo.

Hii ni mara ya kwanza kanisa Katoliki linashambuliwa tangu pale Burkina Faso ilipoanza kukabiliwa na Ugaidi. Rais wa Burkina Faso Roch Marc Christian Kabore ametuma salaam za rambirambi kwa familia huku akiwataka wananchi kuwa waangalifu katika kipindi hiki.