Sita wauawa katika makabiliano Khartoum
Watu sita - askari mmoja na waandamanaji watano - wameuawa Jumatatu jioni wiki hii katika mji mkuu wa Sudani, Khartoum, saa chache baada ya kutangazwa makubaliano kati ya wawakilishi wa maandamano ya kiraia na maafisa wa jeshi wanaoshikilia madaraka kuhusu muundo wa serikali ya mpito nchini humo.
Imechapishwa:
Pande hizo mbili zilianza tena mazungumzo Jumatatu Mei 13, mazungumo ambayo yanaelezwa kuwa muhimu kwa mustakabali wa Sudani, baada ya miongo mitatu ya utawala wa rais wa zamani Omar Hassan al-Bashir, bila hata hivyo kugawana madaraka.
Mapema Jumatatu, Mwanasheria Mkuu wa Sudani alitangaza kumfungulia mashtaka Omar al-Bashir, aliyetimuliwa mamlakani tarehe 11 Aprili mwaka huu na ambaye kwa sasa anazuiliwa jela jijini Khartoum, kwa "mauaji ya waandamanaji" wakati wa maandamano dhidi ya utawala wake.
"Watu wasiojulikana ambao walitaka kuvuruga mazungumzo kati ya pande mbili" walifyatua risasi mbele ya makao makuu ya jeshi la Sudan, ambako waandamanaji wanapiga kambi kwa zaidi ya mwezi mmoja, na kuua kamanda wa kijeshi na kujeruhi askari watatu, pamoja na waandamanaji kadhaa na raia, Baraza la Jeshi limesema.
Katika mkutano na waandishi wa habari Jumatatu usiku, Baraza la Jeshi limesema kuwa "watu wenye silaha waliripotiwa miongoni mwa waandamanaji". Kwa mujibu wa vyanzo vya hospitali vinavyounga mkono maandamano, waandamanaji watano wameuawa, ikiwa ni pamoja na mmoja ambaye ameuawa mbele ya makao makuu ya jeshi.
"Katika mkutano wa leo (Jumatatu), tumekubaliana mfumo wa uundwaji wa taaasisi za serikali ya mpito," msemaji wa waandamanaji Taha Osman ameliambia shirika la Habari la AFP.
"Mazungumzo ya leo Jumanne yatahusu muda wa kipindi cha mpito na muundo wa serikali (mpya)" na taasisi ya Bunge na Baraza la Seneti, kwa mujibu wa Taha Osman.
Msemaji wa Baraza la Jeshi, Jenerali Chamsedddine Kabbachi, amethibitisha makubaliano hayo.