SUDAN-MAANDAMANO-MAZUNGUMZO

Mazungumzo kati ya waandamanaji na viongozi wa kijeshi yakwama nchini Sudan

Viongozi wa kijeshi na waandamanaji wameshindwa kuelewana kuhusu muundo wa serikali ya mpito itakayokuwa madarakani kwa miaka mitatu ijayo baada ya kuondolewa madarakani kwa rais wa zamani Omar al Bashir.

Viongozi wa kijeshi nchini Sudan
Viongozi wa kijeshi nchini Sudan ASHRAF SHAZLY / AFP
Matangazo ya kibiashara

Utata mkubwa ni kuhusu ni nani ataongoza serikali hiyo, baada ya pande zote kuonekana kutokuwa tayari kulegeza kamba.

Mazungumzo hayo yalianza Jumapili iliyopita, karibu mwezi mzima baada ya rais  al-Bashir kuondolewa madarakani na kuzua mwamko mpya wa kisiasa.

Pande zote mbili hazijasema mazungumzo hayo yataendelea tena lini, lakini waandamanaji wamekataa kuondoka katika makao makuu ya jeshi hadi suluhu lipatikane.

Pande zote mbili zimekuwa zikitaka ushiriki kikamilifu katika baraza jipya litakalotawala Sudan kwa miaka mitatu ijayo.

Majadiliano ya hivi karibuni, yamekuja  kufuatia shinikizo kutoka kwa mataifa yenye nguvu duniani kuundwa kwa baraza la kiraia litakalotawala,ambalo ndio moja kati ya matakwa muhimu ya waandamanaji.

Shirikisho la Wahadhiri wa chuo kikuu nchini Sudan ambalo lilianzisha kampeni ya maandamano dhidi ya Bashir mwezi Desemba, lilisema kuwa halina haraka ya kuhitimisha makubaliano hayo.