SUDAN

Maelfu waitikia wito wa mgomo wa nchi nzima Sudan

Maelfu ya wafanyakazi nchini Sudan wameanza mgomo wa nchi nzima, mgomo ambao umesababisha usafiri wa anga na ardhini kusimama huku mamilioni ya raia wakishindwa kusafiri.

Waandamanaji wa Sudan wakiwa na mabango katika moja ya maandamano yao ya hivi karibuni.
Waandamanaji wa Sudan wakiwa na mabango katika moja ya maandamano yao ya hivi karibuni. Photo: AFP
Matangazo ya kibiashara

Mgomo huu ni sehemu ya shinikizo la waandamanaji wanaolitaka jeshi likabidhi madaraka kwa utawala wa kiraia.

Tofauti na hofu iliyokuwepo awali, wafanyakazi karibu nchi nzima wameitikia wito wa viongozi wa waandamanaji ambao waliwataka waanze mgomo kuanzia leo na keshi kuweka shinikizo zaidi kwa jeshi.

Viongozi walio chini ya mwavuli wa waandamanaji, The Alliance for Freedom and Change na wanajeshi ambao walichukua madaraka mwezi mmoja uliopita baada ya kumuondoa Omar al-Bashir, wameshindwa kuondoa tofauti zao kuhusu nani aongoze kamati mpya ya uongozi wa mpito.

Baraza jipya la uongozi linatarajiwa kuongoza kwa muda wa miaka mitatu wakati likianza kuweka utawala wa kiraia ambao utaandaa mazingira ya kufanya uchaguzi mkuu wa kwanza baada ya uongozi wa Bashir.

Katika jaribio lao la kuongeza shinikizo zaidi dhidi ya watawala wa kijeshi, viongozi wa waandamanaji wameitisha maandamano ya siku mbili nchi nzima kuanzia Jumanne.

"Muitikio wa maandamano ya kitaifa umekuwa mzuri kuliko ilivyotarajiwa," amesema kiongozi wa waandamanaji Saddiq Farukh.

"Farukh ameongeza kuwa "maandamano ya siku mbili yanalenga kuwasilisha ujumbe kwa dunia nzima kuwa wananchi wa Sudan wanataka mabadiliko ya kweli na hawataki uongozi wa kijeshi."

Jumatatu ya wiki hii kiongozi wa maandamano Wajdi Saleh aliwaambia waandishi wa habari kuwa mpaka sasa hakuna muafaka wowote uliofikiwa na viongozi wa kijeshi ili kumaliza mvutano uliopo.

Viongozi wa maandamano wanasema wanatarajia madaktari, wanasheria, waendesha mashtaka, waajiriwa wa sekta ya uma, reli, mawasiliano na anga wote watashiriki mgomo wa nchi nzima.

Hata hivyo viongozi wa waandamanaji wanatarajiwa kupata pigo baada ya chama kikuu cha upinzani ya Umma juma hili kutangaza wazi kutounga mkono mgomo wa nchi nzima ulioitishwa, tangazo ambalo lilidhihirisha kuwepo kwa mgawanyiko.