MALAWI

Malawi: Rais Mutharika atangazwa mshindi wa uchaguzi wa juma lililopita

Rais wa Malawi, Peter Mutharika akiwapungia wafuasi wake kwenye moja ya mikutano yake mwezi April.
Rais wa Malawi, Peter Mutharika akiwapungia wafuasi wake kwenye moja ya mikutano yake mwezi April. AMOS GUMULIRA / AFP

Rais wa Malawi, Peter Mutharika amechaguliwa kwa muhula mwingine katika uchaguzi ambao umeshuhia akipata ushindi mwembamba dhidi ya mpinzani wake wa karibu huku matokeo yake yakipingwa na upinzani.

Matangazo ya kibiashara

Matokeo haya ya mwisho yametangazwa baada ya mahakama kuu kuondoa makataa yake ya mwishoni mwa juma ambapo iliagiza tume ya uchaguzi kutotangaza matokeo hayo baada ya kinara wa upinzani Lazarus Chakwera kwenda kulalamika.

Saa chache tu baada ya mahakama kuondoa makataa yake, mwenyekiti wa tume ya uchaguzi nchini Malawi, alimtangaza Mutharika anayeoongoza chama cha Democratic Progressive kama mshindi kwa kupata asilimia 38.57 ya kura zote akifuatiwa na mpinzani wake wa karibu Chakwera anayeongoza chama cha Malawi Congress aliyepata asilimia 35.41 ya kura zote.

Wagombea hawa wametofautiana kwa chini la kura laki moja na elfu 59, huku idadi ya watu waliojitokeza kushiriki ikirekodiwa kuwa asilimia 74 sawa na watu milioni 6 na laki 8.

"Huu ni uamuzi wa wananchi wengi wa Malawi na ni lazima tukubali kwa uungwana," alisema mwenyekiti wa tume ya uchaguzi Jane Ansah.

Msemaji wa chama tawala Nicholas Dausi amenukuliwa na vyombo vya habari akisema "haki imepatikana, na wananchi wameongea."

Hata hivyo matokeo haya yanapingwa vikali na mgombea wa upinzani Chakwera ambaye tangu awali alionya kuhusu uwepo wa njama za kuiba kura, akisisitiza kuwa vituo vyao vinaonesha alikuwa akiongoza.

Tume ya uchaguzi iliacha kutangaza matokeo ya awali Ijumaa ya wiki iliyopita baada ya kupokea malalamiko zaidi ya 147 kutoka kwa vyama vya siasa ambavyo vilikuwa vinapinga matokeo.

Chakwera alienda mahakamani akidai kuwa kulikuwa na udanyanyifu wa matokeo katika karatasi za ujumuishaji kutoka katika majimbo 10 kati ya 28.

Vyama vya upinzani vinalalamika kuwa karatasi za ujumuishaji matokeo zilikuwa zimefanyiwa marekebisho kwa kutumia wino maalumu.