BOTSWANA

Rais wa zamani wa Botswana atangaza kuunga mkono upinzani

Rais wa zamani wa Botswana, Ian Khama.
Rais wa zamani wa Botswana, Ian Khama. wikipedia

Rais wa zamani wa Botswana, Ian Khama ametangaza kuunga mkono upinzani katika uchaguzi mkuu ujao dhidi ya chama tawala cha Botswana Democratic.

Matangazo ya kibiashara

Khama ambaye alikabidhi madaraka kwa aliyekuwa makamu wake wa rais Mokgweetsi Masisi mwaka uliopita baada ya kuhudumu kwa karibu mwongo mmoja, tangu wakati huo alitangaza kujitoa ndani ya chama tawala.

Mzozo wa kisera kati yake na mrithi wake umeendelea kukita mizizi na kutishia mustakabali wa chama tawala ambacho kimekuwa madarakani tangu nchi hiyo ipate uhuru wake mwaka 1966.

Masisi ambaye ni mtu wa tatu kutoka nje ya kundi la Khama kuongoza nchi hiyo tangu uhuru wake kutoka kwa Uingereza, amekuwa akivutana mara kadhaa na mtangulizi wake.

Mvutano wa hivi karibuni ulitokana na uamuzi wa rais Masisi kuamua kuondoa makataa ya uwindaji iliyokuwa imewekwa na rais Khama mwaka 2014.

Akizungumza mwishoni mwa juma na wafuasi wake Khama alisema ataunga mkono upinzani kupitia chama cha Umbrella for Democratic Change wakati wa uchaguzi mkuu wa mwezi October.

"Nimekuja kuwataarifu kuwa naachana na chama cha BDP na sikitambui tena chama hichi, ilikuwa ni kosa kubwa kumchagua Masisi kama mrithi wangu. Sasa nitafanya kazi na upinzani kuhakikisha kuwa BDP inapoteza kwenye uchaguzi wa October," alisema Khama.

Khama alihudumu kwa mihula miwili kama rais kabla ya kuondoka na kumuachia mrithi wake aliyemchagua kutokana na kulazimika kufanya hivyo kama mrithi.

Katika uchaguzi wa mwaka 2014, chama cha BDP kilichindwa kwa mara ya kwanza kupata ushindi wa jumla wakati kikiendelea kujaribu kukabiliana na changamoto za kichumi.