NIGERIA

Buhari ala kiapo kwa muhula wa pili, asisitiza vita dhidi ya rushwa

Rais wa Nigeria, Muhammadu Buhari ameapishwa kuhudumu kwa muhula wa pili, akiapa kwa mara nyingine kuzidisha kasi ya mapambano dhidi ya rushwa na hali tete ya usalama.

Rais wa Nigeria, Muhammadu Buhari akitia saini kiapo kutumikia kwa muhula wa pili. 29 Mei 2019
Rais wa Nigeria, Muhammadu Buhari akitia saini kiapo kutumikia kwa muhula wa pili. 29 Mei 2019 REUTERS/Afolabi Sotunde
Matangazo ya kibiashara

Buhari mwenye umri wa miaka 76 amekuwa madarakani tangu mwaka 2015, alichaguliwa kwa muhula mwingine mwezin February, amekula kiapo kuhudumu kwa muhula wa pili kwa kipindi cha miaka 4 jijin Abuja.

"Naapa ya kwanza, nitakuwa muaminifu na mzalendo kwa jamhuri ya Nigeria," alisema rais Buhari ambaye alikuwa amevalia vazi la kawaida la kitamaduni ambapo aliongeza kuwa "Nitahifadhi, kuilinda na kuitetea katiba."

Rais Buhari amekula kiapo katika shughuli ambayo maofisa wake wamesema ni sherehe isiyo ya shamrashamra nyingi kama ambavyo imezoeleka.

Makamu wa rais Yemi Osinbajo nae aliapishwa hivi leo kuingia ofisini.

Buhari alichaguliwa tena kwa kupata ushindi wa asilimia 56 ya kura zote, uchaguzi uliofanyika baada ya kuahirishwa kwa juma moja kutokana na maandalizi hafifu.

Pingamizi la upinzani

Mpinzani wake, Atiku Abubakar wa chama cha Peoples Democratic PDP, ambaye alimaliza katika nafasi ya pili kwa kupata asilimia 41 ya kura zote, yeye pamoja na wanasiasa wengine wa upinzani wamefungua kesi kupinga ushindi wake.

Abubakar na wenzake wanadai kuwa kulikuwa na dosari nyingi wakati wa uchaguzi, wakiuita uchaguzi ule kama "aibu".

Rais Buhari, afisa wa zamani katika jeshi kwenye miaka ya 1980, ameapa kuhakikisha nchi yake inasalia salama dhidi ya makundi ya kijihadi.

Kiongozi huyu hata hivyo anaanza muhula wake wa pili na wa mwisho huku taifa hilo lilikabiliwa na changamoto nyingi zikiwemo za usalama, rushwa, ukosefu wa ajira na mgawanyo usio sawa wa rasilimali.

Wakati wa uongozi wake mara kadhaa watu walihoji utimamu wake wa kuendelea kuongoza baada ya mara kadhaa kufanya safari za nje ya nchi kwaajili ya matibabu.

Katika sheria za mwaka huu hakukuwa na kiongozi yoyote wa bara la Afrika aliyealikwa.