BURUNDI

Burundi yatishia kusitisha uhusiano na mjumbe wa umoja wa Mataifa

Rais wa Burundi, Pierre Nkurunziza. Picha ya maktaba Julai 7, 2018
Rais wa Burundi, Pierre Nkurunziza. Picha ya maktaba Julai 7, 2018 REUTERS/Evrard Ngendakumana

Nchi ya Burundi inatishia kusitisha ushirikiano na mjumbe maalumu wa umoja wa Mataifa kwa nchi hiyo, utawala wa Bujumbura ukieleza kutoridhishwa na namna mjumbe huyo amekuwa akiingilia masuala yake ya ndani.

Matangazo ya kibiashara

Katika tukio la kushtukiza baraza la usalama la umoja wa Mataifa lilisitisha kikao chake cha siku ya jumanne ya wiki hii kuijadili Burundi, baada ya utawala wa Bujumbura kudai kuwa uko tayari kusitisha ushirikiano na Michel Kafando.

Kafando ambaye ni rais wa zamani wa Burkina Fasi, alchaguliwa mwaka 2017 kuongoza juhudi za kusaka suluhu ya kisiasa nchini Burundi, taifa ambalo limekumbwa na mizozo tangu kumalizika kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe mwaka 2006.

Matamshi ya Burundi yamekuja wakati huu nchi hiyo ikijiandaa kwa uchaguzi wake mkuu hapo mwakani.

Nchi ya Ufaransa iliomba kufanya mkutano wa faragha Ijumaa ya wiki hii, lakini hata hivyo mkutano huo ukalazimika kusogezwa mbele hadi mwezi Juni ili kujaribu kutuliza hali ya mambo.

Akiulizwa na wanahabari kuhusu mvutano uliopo kati ya Serikali ya Burundi na mjumbe wa umoja wa Mataifa kwa nchi hiyo, msemaji wa umoja wa Mataifa Farhan Haq amesema hakuwa na taarifa za tangazo lolote rasmi kutoka kwa Serikali ya Burundi.

Nchi ya Burundi imekuwa kwenye mzozo tangu rais Pierre Nkurunziza awanie kiti cha urais kwa muhula wa 3 ambapo alichaguliwa mwaka 2015 katika uchaguzi uliosusiwa na upinzani.

Watu wanaokadiriwa kufikia elfu 1 na 200 wamepoteza maisha na wengine zaidi ya laki 4 wamekimbia nchi yao kutokana na machafuko ya mara baada ya uchaguzi wa mwaka 2015 na mwezi May mwaka 2017, mauaji ambayo umoja wa Mataifa unasema yalitekelezwa na vikosi vya Serikali.

Hata hivyo katika hatua ya kushangaza, mwaka uliopita rais Nkurunziza alitangaza kuwa hatowania kiti cha urais katika uchaguzi mkuu wa mwakani, akienda tofauti na wakosoaji wake waliokuwa wakimuona kama anapanga njama za kujiongezea muda kusalia madarakani.

Balozi wa Burundi kwenye umoja wa Mataifa, Albert Shingiro tangu wakati huo amekuwa akilitaka baraza la usalama kusitisha vikao vyake vya kila mwezi kuijadili nchi yake.