DRC

Viongozi 6 wa Afrika kuhudhuria mazishi ya Etienne Tshisekedi

Mwili wa Etienne Tshisekedi ukiwa katika uwanja wa Stade des Martyrs ambapo wananchi wanatoa heshima za mwisho. 31 MAY 2019
Mwili wa Etienne Tshisekedi ukiwa katika uwanja wa Stade des Martyrs ambapo wananchi wanatoa heshima za mwisho. 31 MAY 2019 RFI

Maelfu ya raia nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, wameendelea kutoa heshima za mwisho kwa mwili wa aliyekuwa kinara wa upinzani na wakati mmoja waziri mkuu wa nchi hiyo, Etienne Tshisekedi.

Matangazo ya kibiashara

Mwili wa Tshisekedi uliwasili nchini DRC Alhamisi ya wiki hii ukitokea nchini Ubelgiji ambako ulikuwa umehifadhiwa kwa zaidi ya miaka miwili.

Mwili wa Tshisekedi uliwasili kwenye uwanja wa ndege wa Kinshasa maajira ya saa moja na dakika 20 usiku na kupokelewa na viongozi kadhaa wa Serikali pamoja na wananchi waliokuwa nje ya uwanja kuusubiri mwili wake.

Tshisekedi alifariki akiwa mjini Brussels mwezi February mwaka 2017 akiwa na umri wa miaka 84, ambapo ameshindw akushuhudia kuapishwa kwa mwanawe Felix Tshisekedi ambaye amekuwa rais wa DRC kupitia uchaguzi mkuu wa mwaka jana.

Felix aliahidi kuurejesha nyumbani mwili wa baba yake na kuuzika katika eneo stahili, akitimiza ahadi ambayo alishindwa kuifanya wakati wa utawala wa rais Joseph Kabila.

Baada ya kuchelewa kuondoka mjini Brussels siku ya Jumatano, hatimaye mwili wake ulisafirisha siku ya Alhamisi na kuwasili jijini Kinshasa usiku.

Mtoto wake Felix aliongoza ujumbe wa viongozi wengine kuupokea mwili wa baba yake.

Jeneza jeupe lililofunikwa na bendera za taifa, lilitolewa katika ndege na askari kuupokea na kisha kuupakia kwenye gari maalumu.

Mwili wa Tshisekedi umewekwa katika uwanja wa mpira wa Stade Martyr ambapo wananchi wanapata nafasi ya kutoa heshima za mwisho kabla ya mazishi yake hapo kesho kwenye mji wa Nsele nje kidogo ya jiji la Kinshasa.

Jumla ya viongozi 6 wa Afrika wanatarajiwa kuhudhuria mazishi yake akiwemo rais wa Angola, rais wa Rwanda Paul Kagame, rais wa Togo na nchi jirani ya Congo Brazzaville.