ZIMBABWE-EU-UCHUMI-VIKWAZO

Zimbabwe yaanza mazungumzo na mataifa ya EU kuiondolea vikwazo

Rais wa Zimbabwe  Emmerson Mnangagwa
Rais wa Zimbabwe Emmerson Mnangagwa REUTERS/Philimon Bulawayo

Nchi ya Zimbabwe na umoja wa Ulaya zimeanza mazungumzo rasmi ya kisiasa baada ya miaka takribani 17 ya sintofahamu wakati wa uongozi wa rais wa zamani Robert Mugabe.

Matangazo ya kibiashara

Mabalozi kutoka nchi za umoja wa Ulaya walioko Zimbabwe wamekutana na wawakilishi wa Serikali katika awamu ya kwanza ya mfululizo wa mazungumzo yaliyopangwa kufanyika baina ya pande hizo mbili kujaribu kumaliza miongo kadhaa ya vikwazo vya kiuchumi kwa Zimbabwe.

Umoja wa Ulaya uliondoa sehemu kubwa ya vikwazo vya kiuchumi kwa nchi ya Zimbabwe mwaka 2014 lakini imekuwa haitoi msaada wa kifedha kwa Serikali.

Hatua hii imekuja, baada rais wa Marekani Donald Trump, mapema mwaka huu kuongeza vikwazo vya muda wa mwaka mmoja zadi kwa taifa hilo la Kusini mwa Afrika.

Uongozi wa rais Trump unasema kuwa, sera za serikali ya rais Emmerson Mnangagwa bado ni hatari kwa sera yake ya mambo ya nje.

Mataifa ya Afrika yakiongozwa na Afrika Kusini, yameendelea kutaka Mataifa ya Magharibi kuiondolea vikwazo Zimbabwe ili kuipa nafasi ya kukua tena kiuchumi.