Pata taarifa kuu
SUDAN

Mjumbe wa Serikali ya Marekani atarajiwa Sudan, hali bado tete

Mtoto raia wa Sudan akionesha alama ya vema mjini Khartoum Juni 2 mwaka 2019, waandamanaji bado wameweka vizuizi kuelekea makao makuu ya jeshi.
Mtoto raia wa Sudan akionesha alama ya vema mjini Khartoum Juni 2 mwaka 2019, waandamanaji bado wameweka vizuizi kuelekea makao makuu ya jeshi. ASHRAF SHAZLY / AFP
Ujumbe kutoka: Emmanuel Richard Makundi
2 Dakika

Afisa wa juu kutoka Serikali ya Marekani anatarajiwa kufanya ziara juma hili nchini Sudan ambapo anakwenda kujaribu kutafuta suluhu ya mzozo wa kisiasa ambao umesababisha vifo vya watu zaidi ya 100 tangu juma lililopita.

Matangazo ya kibiashara

Ziara ya Tibor Nagy naibu katibu mkuu anayehusika na masuala ya Afrika, inakuja wakati huu ambapo waandamanaji nchini Sudan wameanza mgomo wa nchi nzima kutotii Serikali.

Akiwa nchini Sudan, Nagy anatarajiwa kukutana na viongozi wa baraza la kijeshi na wale viongozi wa waandamanaji.

Nagy ataondoka nchini Sudan Jumatano ya wiki hii ambapo ataelekea Ethiopia kukutana na waziri mkuu Abiy Ahmed pamoja na wakuu wa umoja wa Afrika mjiji Addis Ababa.

Taarifa ya Serikali ya Washington imesema kuwa mwanadipolomasia huyo anatarajiwa kutoa wito wa usitishwaji wa makabiliano kati ya vyombo vya usalama na waandamanaji na kutaka kufanyike kwa mazungumzo mapya.

Waandamanaji ambao wamekuwa wakipiga kambi nje ya makao makuu ya jeshi mjini Khartoum wakishinikiza kuwekwa kwa utawala wa kiraia, wamekuwa wakiondolewa kwa nguvu na wanajeshi wa Serikali tangu wiki iliyopita ambapo mamia ya watu walipoteza maisha.

Kwa mujibu wa kamati ya madaktari ambao wako karibu na waandamanaji, inasema zaidi ya watu 118 wameuawa tangu kuanza kwa operesheni ya kuwaondoa waandamanaji walioweka vizuizi kuzingira makao makuu ya jeshi.

Jumatatu ya wiki hii viongozi wa baraza la kijeshi walidai kuwa maofisa kadhaa wa jeshi wamekamatwa wakihusishwa na tukio la mauaji ya raia juma lililopita.

Haya yanajiri wakati huu ambapo viongozi wa waandamanaji wamekataa wito wa kurejea kwenye mazungumzo wakisema wanajeshi walioko hawaaminiki wakitaka kwanza maofisa waliohusika na mauaji ya raia wakamatwe pamoja na kuachiwa huru kwa wafungwa wote wa kisiasa.

Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.