MALI-SIASA-USALAMA-MAUAJI

Watu wenye silaha wawauwa watu 38 nchini Mali

Vikosi vya usalama nchini Mali
Vikosi vya usalama nchini Mali Olivier Fourt

Watu 38 wameuawa na wengine kujeruhiwa nchini Mali baada ya kuzuka kwa mapigano ya kikabila katika vijiji vya Dogon, katikati ya nchi hiyo.

Matangazo ya kibiashara

Hakuna kundi lolote lililodai kutekeleza mauji haya mabaya ambayo yametokea siku ya Jumatatu kati ya kabila la Dogon na Fulani.

Serikali ya Mali imethibitisha kutokea kwa mauaji hayo na kusema, watu wenye silaha, walilenga vijiji vya Gangafani na Yoro, karibu na mpaka wa Burkina Faso.

Mapema mwezi Juni, watu wengine 35 walipoteza maisha baada ya watu wenye silaha kuvamia kijiji cha Dogon katika eneo la Sobane Da, mashambulizi ambayo yameelezwa pia ni ya kikabila.

Licha ya rais Boubacar Keita kutembelea eneo la mauaji hayo na kutoa wito wa utulivu na kukomeshwa kwa mauaji, hayo yameendelea kutokea mara kwa mara.

Tangu mwaka 2012, tangu kuzuka kwa makundi ya kijihadi na waasi wa Tuareg, nchi ya Mali imeendelea kukabiliana na changamoto za kiusalama, licha ya kuwa na msaada wa kijeshi kutoka Ufaransa na kwa Umoja wa Mataifa.