MALAW-MAANDAMANO-UPINZANI-URAIS

Maelfu ya wafuasi wa upinzani waandamana nchini Malawi, kulalamikia wizi wa kura

Maelfu ya wafuasi wa upinzani, wamekuwa wakiandamana nchini Malawi, kulalamikia matokeo ya Uchaguzi Mkuu uliofanyika mwezi Mei, na rais Peter Mutharika kutangazwa mshindi.

Maandamano ya upinzani nchini Malawi
Maandamano ya upinzani nchini Malawi Voa
Matangazo ya kibiashara

Wafuasi hao kutoka chama cha MCP na kile cha UTM wanapinga ushindi wa Mutharika, na kuendelea kudai  kuwa mgombea mkuu wa upinzani Lazarus Chakwera aliibiwa kura.

Maandamano hayo yaliyohudhuriwa na maelfu ya waandamanaji, yamefanyika jijini Lilongwe, Blantyre na Zomba.

Wakati wa maandamano hayo, waandamanaji waliimba nyimbo za kumsifu Chakwera na kumtaka Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Jane Ansah, kujiuzulu.

Mbali na maandamano hayo, upinzani umekwenda Mahakamani kupinga ushindi wa rais Mutharika na Majaji wanatarajiwa kutoa uamuzi siku ya Ijumaa wiki hii.

Rais Mutharika ambaye tayari ameanza muhula wa pili, alipata ushindi mwembamba kwa kupata kura 1,940,709 dhidi ya mpinzani wake aliyepata kura 1,781,740.