LIBYA-UTURUKI-HAFTAR-USALAMA

Mvutano waongezeka kati ya Ankara na Marshal Haftar, Libya

Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki Mevlut Cavusoglu, Jeddah, Saudi Arabia, Mei 29, 2019.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki Mevlut Cavusoglu, Jeddah, Saudi Arabia, Mei 29, 2019. REUTERS/Waleed Ali/File Photo

Uturuki imeendelea kushtumu majeshi yanayomtii Marshal Khalifa Haftar kuwashukilia Waturuki sita nchini Libya, na kutishia kuchukua hatua ikiwa raia wake hawatoachiwa huru.

Matangazo ya kibiashara

Tukio hilo linakuja siku mbili baada ya Marshal Haftar kutishia kushambulia makampuni, ofisi na mali za Uturuki nchini nchini Libya, akishtumu Ankara kwamba inaunga mkono mahasimu wake wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa inayotambuliwa na jumuiya ya kimataifa.

Mvutano huo unaendelea kuongezeka kila kukicha kati ya Ankara na Marshal Khalifa Haftar. Katika taarifa, Wizara ya Mambo ya Nje ya Uturuki inashutumu mbabe wa kivita nchini Libya Marshal Khalifa Haftar kuwa yeye na wanamgambo wake haramu wanajihusisha na "vitendo vya ukatili na uharamia.

Ankara imeomba raia wake sita wanaoshikiliwa na vikosi vinavyomtii Marshal Haftar waachiwe huru mara moja na kutishia, ikiwa hilo halitofanyika, kuanza kushambulia vikosi hivyo.

Saa chache kabla, Waziri wa Ulinzi wa Uturuki alionya kwamba nchi yake itajibu dhidi ya shambulio lolote la majeshi ya Haftar.

Hata hivyo Marshal Haftar aliagiza vikosi vyake kufanya mashambulizi dhidi ya meli na mali nyingine za Uturuki na kuwakamata raia wa Uturuki nchini Libya.

Marshal Haftar anashtumu Ankara kusaidia kijeshi mahasimu wake wa Serikali ya Umoja wa kitaifa (GNA). Siku kumi zilizopita, Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan alithibitisha kuwa nchi yake ilitoa msaada wa silaha kwa serikali ya Libya inayoungwa mkono na jumuiya ya kimataifa.

Tangu mwaka wa 2011, hata hivyo, Umoja wa Mataifa uliweka marufu ya kuuzia silaha Libyalicha yakuwa, marufuku hiyo imekuwa ikikiukwa mara kadhaa katika miaka ya hivi karibuni.