DRC-LAMUKA-SIASA

DRC: Mvutano waibuka kati ya wafuasi wa Katumbi na Fayulu

Gavana wa zamani wa Katanga Moïse Katumbi (kushoto) na kiongozi wa upinzani Martin Fayulu, aliyekuwa mgombea wa upinzani katika uchaguzi wa urais wa 2018 nchini DRC.
Gavana wa zamani wa Katanga Moïse Katumbi (kushoto) na kiongozi wa upinzani Martin Fayulu, aliyekuwa mgombea wa upinzani katika uchaguzi wa urais wa 2018 nchini DRC. © AFP/Fabrice Coffrini/Luis Tato

Wafuasi wa gavana wa zamani wa Katanga Moïse Katumbi Chapwe wamelaani hatua ya Martin Fayulu ya kuchapisha taarifa bila makubaliano na kiongozi wao.

Matangazo ya kibiashara

Hali hiyo inajiri wakati Martin Fayulu na Moise Katimbi Chapwe walisaini taarifa inayotoa wito wa maandamano Juni 30. Wamekuwa hawaelewani kwa miezi kadhaa kuhusu mkakati wa kutumia dhidi ya rais Felix Tshisekedi.

Olivier Kamitatu, mkurugenzi wa ofisi ya Moïse Katumbi, hakukubaliana na taarifa hiyo kwa niaba ya muungano wa vyama vya upinzani Lamuka, taarifa ambayo haikuwekwa saini na viongozi wake.

"Si jambo la kawaida," ameandika kwenye ukurasa wake wa Twitter.

Hata hivyo, Olivier Kamitatu anasema ameshangazwa na ujumbe wa Martin Fayulu alioandika kwenye ukurasa wake wa Twitter unaopendekeza msaada kutoka kwa rais Felix Tshisekedi.

Kamitatu anasema: Martin Fayulu kupendekeza "mazungumzo" na rais, inamaanisha kuwa amebadili kauli yake ya kupinga matokeo ya uchaguzi na badala yake amekubali kuwa uchaguzi ulikuwa wa haki, huru na wa wazi, na kukubali kuwa Felix Tshisekedi ni mshindi halali wa uchaguzi wa urais.

"Katumbi na Fayulu wanapaswa kuketi kwenye meza ya mazungumzo ili kuona kama bado wanataka kufanya kazi pamoja," amesema mshirika wa karibu wa gavana wa zamani, akimshtumu Martin Fayulu na washirika wake kwenda mbali kwa kumshambulia hadharani Moise Katumbi.

Mmoja wa washirika wa Martin Fayulu ametaja hali hiyo kama jaribio la "kupotosha" wafuasi wake kutoka katika vita yao na hali inayojiri kwa sasa, ambayo ni "kukupinga uhalifu wa polisi dhidi ya maandamano ya raia yaliyofanyika Jumatatu wiki hii."