LIBYA-USALAMA

Wahamiaji zaidi ya arobaini waangamia katika shambulio Libya

Wahamiaji wa Afrika wakikusanyika nje ya kituo cha Tajoura.
Wahamiaji wa Afrika wakikusanyika nje ya kituo cha Tajoura. © AFP

Wahamiaji zaidi ya arobaini wameuawa katika shambulio la anga dhidi ya kambi yao katika moja ya vitongoji vya mji wa Tripoli, mji unaokabiliwa na mashambulizi ya wapiganaji wa Marshal Khalifa Haftar.

Matangazo ya kibiashara

Watu 70 wamejeruhiwa katika shambulio hilo katika kitongoji cha Tajoura, kulingana na ripoti ya awali kutoka idara ya huduma za dharura.

Msemaji wa huduma za dharura nchini Libya Osama Ali ameliambia shirika la habari la AFP kwamba hiyo ni ripoti ya awali na idadi ya waliofariki inaweza kuongezeka.

“Wahamiaji 120 walikuwa wanazuiliwa katika jengo la kuhifadhi ndege ambalo limeshambuliwa. Miili ya watu imetapakaa sakafuni katika jengo hilo,” amesema Bw Ali.

Mpiga picha wa shirika la habari la AFP, ambaye yuko eneo la tukio anasema, maafisa wa idara ya huduma za dharura wanaendelea na shughuli ya kutafuta watu walionurusika ambao wamekwama chini ya kifusi, huku magari ya wagonjwa yakiendelea kuwasili katika eneo la tukio.