Mvutano wajitokeza katika muungano wa wa FCC
Imechapishwa:
Nchini Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo kumezuka mgawanyiko ndani ya Muungano wa FCC unaoungwa mkono na rais mstaafu wa nchi hiyo, Joseph Kabila, punde baada ya uteuzi wa Seneta Alexis Thambwe Mwamba, kuwa mgombea wa nafasi ya Rais wa Baraza la Seneti nchini humo.
Awali muungano huo ulimpendekeza rais mstaafu Joseph Kabila, lakini baada ya mkutano mkuu wa viongozi wanachama wa muungano wa FCC ikaamliwa kuwa ateuliwe mtu mwengine.
Chama cha AFDC, moja kati ya vyama vinavyounda muungano huo, kimesema kiongozi wake Bahati Lukwebo ndiye mtu anayefaa kwa nafasi hiyo, hatua ambayo naonyesha huenda kukashuhudiwa mvutano mkubwa wa kisiasa ndani ya FCC.
Hayo yanajiri wakati muungano mwengine wa upinzani wa Lamuka unakabiliwa na mgawanyiko mkubwa, baada ya kujitokeza mvutano kati ya wafuasi wa Moise Katumbi Chapwe na Martin Fayulu.
Wafuasi wa gavana wa zamani wa Katanga Moïse Katumbi Chapwe wamelaani hatua ya Martin Fayulu ya kuchapisha taarifa bila makubaliano na kiongozi wao.
Hali hiyo inajiri wakati Martin Fayulu na Moise Katimbi Chapwe walisaini taarifa inayotoa wito wa maandamano Juni 30. Wamekuwa hawaelewani kwa miezi kadhaa kuhusu mkakati wa kutumia dhidi ya rais Felix Tshisekedi.
Mmoja wa washirika wa Martin Fayulu ametaja hali hiyo kama jaribio la "kupotosha" wafuasi wake kutoka katika vita yao na hali inayojiri kwa sasa, ambayo ni "kukupinga uhalifu wa polisi dhidi ya maandamano ya raia yaliyofanyika Jumatatu wiki hii."