MALI-USALAMA

Maafisa wa Mali wanaopinga mchakato wa amani waendelea kukabiliwa na vikwazo

Askari wa kikosi cha Umoja wa Mataifa Mali (Minusma) wakipiga doria (picha ya kumbukumbu).
Askari wa kikosi cha Umoja wa Mataifa Mali (Minusma) wakipiga doria (picha ya kumbukumbu). © AFP/Sebastien Rieussec

Idadi ya watu wanaopinga mchakato wa amani nchini Mali na kuchukuliwa vikwazo na Umoja wa Mataifa inaendelea kuongezeka. Watu watano wanaoshtumiwa kupinga mchakato wa amani nchini humo wametambuliwa na kutajwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Matangazo ya kibiashara

Watu hao wamepigwa marufuku ya kusafiri, hatua iliyochukuliwa kwa raia watatu wa Mali mwezi Desemba mwaka jana.

Ahmed Ag Albachar ni mtu muhimu katika mji wa Kidal, ambaye bado anaongoza wa waasi wa zamani. Umoja wa Mataifa unamtaja kama mfanyabiashara ambaye ana ushawishi mkubwa kwa kupora msaada wa kibinadamu unaopelekwa kwa walengwa, lakini pia kama mwanachama wa kundi la zamani la waasi la CMA mwenye ushawishi mkubwa. Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, anahusika katika mashambulizi dhidi ya Walinda amani, dhidi ya jeshi la Mali na dhidi ya majeshi ya G5 Sahel.

Mtu mwingine muhimu ambaye amechukuliwa vikwazo ni Mohamed Ould Mataly, mbunge aliyechaguliwa kwa tiketi ya chama tawala cha RPM, katika mkoa wa Gao. Anashutumiwa kupinga zoezi la uteuzi wa viongozi wapya katika mkoa huwo wa Gao, na anahusika katika biashara mbalimbali haramu, kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa. Ni mwanachama wa mojawapo ya makundi yenye silaha yanayounga mkono serikali, pamoja na kiongozi mwengine wa kundi la wapiganaji , ambaye pia alihukumiwa, Mahri Sidi Amar Ben Daha.

Watu wengine wawili ambao pia wamezuiliwa kusafiri ni Houka Houka Ag Alhousseini, na Mohamed Ben Ahmed Mahri.