SUDANI-SIASA-USALAMA

Makubaliano ya taasisi za mpito yapatikana kwa shinikizo la kimataifa Sudan

Donald Booth, Mjumbe maalum wa Marekani kwa Sudan, Machi 2015.
Donald Booth, Mjumbe maalum wa Marekani kwa Sudan, Machi 2015. © SAMIR BOL / AFP

Makubaliano ya kuundwa kwa taasisi za mpito nchini Sudan yalipatikana kwa shinikizo la kimataifa. Makubaliano hayo kati ya uongozi wa kijeshi na muungano wa kiraia yalipatikana Julai 5 mwaka huu.

Matangazo ya kibiashara

Makubaliano hayo yanatoa ushirikiano na kugawana madaraka kwenye uongozi wa nchi kwa muda wa zaidi ya miaka mitatu. Kulingana na uchunguzi wa shirika la Habari la Associated Press, shinikizo la kidiplomasia na mikutano ya siri vilifanikisha makubaliano hayo kati ya uongozi wa kijeshi na muungano wa kiraia.

Kwa miezi kadhaa Sudan iliendelea kukumbwa na maandamano yasiyokoma, huku watu kadhaa wakipoteza maisha katika makabiliano kati ya waandamanaji na vikosi vya usalama na ulinzi.

Kwa mujibu wa Associated Press, shinikizo kubwa lilitoka upande wa Washington, kutokana na uteuzi wa Donald Booth kama mjumbe maalum Marekani kwa Sudan Juni 12. Marekani iliweka kwanza shinikizo kwa washirika wao wenyewe, Saudi Arabia, Umoja wa Falme za KIarabu na Misri.

Nchi hizi tatu ni washirika wakuu wa uongozi wa kijeshi nchini Sudan. Saudi Arabia, Umoja wa Falme za KIarabu na Misri waliombwa kuunga mkono mapendekezo ya wapatanishi wa mgogoro huo, Umoja wa Afrika na Ethiopia.

Haijulikani kama mjumbe huyo maalum kwa Sudan alitumia mbinu za shinikizo. Kwa vyovyote vile, ujumbe kama huo ulitolewa kwa jeshi na muungano wa kiraia nchini Sudan. Inawezekana kuwa Washington iliweza hata kutoa ahadi ya kinga kwa askari wanaokabiliwa na hatia ya mauaji ya raia. "Marekani ilikuwa inaomba mkataba haraka iwezekanavyo, chanzo kutoka Sudan kimesema. Ujumbe wao ulikuwa wazi: kugawana madaraka na ushirikiano, hakuna mtu kutoka baraza la kijeshi atakaye fuatiliwa".

"Muafaka ulipatikana Juni 29 wakati wa mkutano wa siri nyumbani kwa mfanyabiashara mmoja nchini Sudan. Wawakilishi wa waandamanaji, Viongozi wa utawala wa kijeshi Abdel Fatah Al Burhan na Hemetti, maafisa kutoka Marekani, Uingereza, nchi kadhaa za Kiarabu na Umoja wa Falme za Kiarabu walikuwa miongoni mwa walioshiriki mkutano huo. Mazungumzo yaliyoelezewa kuwa yenye mvutano yalidumu saa tatu, na hatimaye pande mbili zilifikia makubaliano.

Siku moja baadaye viongozi wa waandamanaji waliendelea kushikilia msimamo wao wa kufanya maandamano makubwa, wakisema wanahitaji muda wa kuandaa wafuasi wao. Siku tano baadaye, makubaliano yalitangazwa.