DRC-USALAMA

Polisi yaendesha operesheni kabambe dhidi ya wahalifu Kinshasa

Jenerali Sylvano Kasongo, mkuu wa polisi wa mji wa Kinshasa, hapa ilikuwa Juni 30, 2019.
Jenerali Sylvano Kasongo, mkuu wa polisi wa mji wa Kinshasa, hapa ilikuwa Juni 30, 2019. © ALEXIS HUGUET / AFP

Polisi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, wiki hii imeendesha operesheni kabambe dhidi ya wahalifu katika mji mkuu wa nchi hiyo, Kinshasa. Polisi imetangaza kwamba imekamata watu zaidi ya mia moja na magari yaliyokuwa yameibiwa.

Matangazo ya kibiashara

Jumatatu, Julai 8, katika wilaya ya Kitambo, vikosi vya usalama vilizingira maeneo kadhaa ya wilaya hiyo, huku vikiendesha ukaguzi katika magari mbalimbali. Madereva walitakiwa kuonyesha leseni zao. Zoezi hilo lilifanyika mchana kutwa hadi usiku, hasa katika mtaa wa Komoriko.

Asubuhi iliyofuata, polisi iliendesha operesheni nyingine katika baadhi ya maeneo ya wilaya ya Lingwala. Watu kadhaa walikamatwa. Kwa mujibu wa Jenerali Sylvano Kasongo, mkuu wa polisi katika mji wa Kinshasa, kutumwa kwa maafisa wa polisi katika maeneo hayo ni katika lengo la kupambana na vitendo vya uhalifu. "Tulilenga maeneo hayo, kwani tulikuwa tayari na majina ya watu na sehemu wanakoishi," amesema Jenerali Kasongo.

Operesheni hiyo kabambe tangu Felix Tshisekedi kuingia madarakani, imewezesha watu zaidi ya mia moja kukamatwa. Kwa mujibu wa polisi, wahalifu mbalimbali ni miongoni mwa watu waliokamatwa: majambazi wenye silaha, wezi wa magari na wahalifu wa mtandao maalumu katika utekaji nyara. Watu hao wataonyeshwa kwa vyombo vy habari leo Ijumaa, kwa mujibu wa chanzo cha polisi.

Polisi imeonya kuwa barabara nyingi zitafungwa katika siku zijazo kwa operesheni kama hiyo, lakini raia watafahamishwa.