DRC-EBOLA-AFYA

Mtu mmoja apatikana na virusi vya Ebola Goma

Wafanyakazi wa kituo kinachotoa hudumu kwa wagonjwa wa Ebola cha Butembo wakimuhudumia mwanamke aliyeambukizwa virusi vya Ebola, Machi 28, 2019.
Wafanyakazi wa kituo kinachotoa hudumu kwa wagonjwa wa Ebola cha Butembo wakimuhudumia mwanamke aliyeambukizwa virusi vya Ebola, Machi 28, 2019. REUTERS/Baz Ratner

Serikali ya DRC imetoa tahadhari kwa raia wa Goma na viunga vyake kuwa mtu mwenye virusi vya Ebola amepatikana baada ya kufanyiwa ukaguzi katika kituo kimoja mjini Goma muda mfupi baada ya kuwasili kutoka Butembo jana Jumapili.

Matangazo ya kibiashara

Kwa mujibu wa wizara ya afya ya DRC, mtu huyo ambaye ni Mchungaji alisafiri umbali wa kilomita zaidi ya 200 kutoka Butembo hadi Goma kwa basi, na inasadikiwa kuwa alikuwa amekutana na watu wenye ugonjwa Ebola.

Hata hivyo wizara ya Afya inasema kwamba hatari ya kusambaa kwa Ebola katika sehemu nyingine za mji wa Goma ni ndogo.

“Dereva wa basi na abiria wengine 18 wanatarajiwa kutpewa chanjo leo Jumatatu”, wizara ya afya imeongeza katika taarifa yake.

Wakaazi zaidi ya milioni moja wanaoishi katika mji wa Goma wameanza kuingiliwa na hofu kwa mujibu wa chanzo kimoja kutoka moja ya mashirika ya kiraia mjini humo.

Ebola huwaathiri binaadamu kupitia mgusano na wanyama walioathirika kama tumbili, na popo wa msituni.

Watu huambukizwa kwa njia ya kugusana, njia ya mdomo na pua, pia kwa njia ya damu, matapishi, kinyesi, majimaji ya kwenye mwili wa mtu mwenye Ebola.

Ebola ni ugonjwa unaoambukizwa na virusi ambapo aliyepata maambukizi hupata dalili za homa, uchovu, maumivu ya viungo na koo.