DRC-EBOLA-SIASA-AFYA

Ebola: Waziri wa Afya wa DRC, Oly Ilunga, ajiuzulu

Waziri wa Afya wa DRC Oly Ilunga achukuwa uamuzi wa kujiuzulu kwenye nafasi yake.
Waziri wa Afya wa DRC Oly Ilunga achukuwa uamuzi wa kujiuzulu kwenye nafasi yake. Dr. Oly Ilunga/twitter.com

Waziri wa Afya wa DRC, Oly Ilunga, amejiuzulu kwenye nafasi yake, akibaini kwamba hakutendewa haki na uamuzi wa rais Tshisekedi wa kusimamia jitihada za kukabiliana na ugonjwa wa Ebola ulioua watu zaidi ya 1,700 ndani ya kipindi cha mwaka mmoja, mashariki mwa DRC.

Matangazo ya kibiashara

"Kwa sababu ya uamuzi wako wa kuweka mikakati dhidi ya virusi vya Ebola chini ya usimamizi wako wa moja kwa moja na kutokana na athari ambazo zinaweza kujitokeza kufuatia uamuzi wako huo, ninawasilisha barua yangu hii ya kujiuzulu kama Waziri wa Afya, "Waziri wa Afya, Dk. Oly Ilunga, ameandika kwenye barua yake leo Jumatatu.

Hatua hii inakuja siku nne baada ya shirika la Afya Duniani (WHO) kutangaza "dharura ya kiafya" duniani kwa sababu ya ugonjwa wa Ebola nchini DRC ambao umeua watu 1,700 tangu mwezi Agosti mwaka jana.

Tahadhari hii ilitolewa baada ya mtu wa kwanza kufariki dunia baada ya kuambukizwa virusi vya Ebola katika mji wa Goma, mji unaotembelewa na watu kutoka nchi mbalimbali za Maziwa Makuu.

Shirika la Afya Duniani linasema virusi vya ugonjwa huo vinaendelea kusambaa kutoka Afrika Magharibi na sasa kufikia nchi nyingine. Mataifa mengi yameimarisha ukaguzi katika viwanja vya ndege.

Lakini shirika hilo limesema hatari ya ugonjwa huo kusambaa nje ya Congo si kubwa.

Mlipuko wa Ebola ni ugonjwa wa pili kwa ukubwa katika historia ya nchi hiyo, ulianza mwezi Agosti na inaathiri mikoa miwili nchini DRC, Kivu Kaskazini na Ituri.

Zaidi ya watu 2500 wameathiriwa na ugonjwa huo na theluthi mbili kati yao wamepoteza maisha.

Ilichukua siku 224 kwa idadi ya walioathirika kufika 1,000 , lakini ndani ya siku 71 zaidi idadi ilifika 2,000.

Watu takribani 12 huripotiwa kupata ugonjwa huo kila siku.

Wafanyakazi wa afya wamekua wakipata vikwazo vya kutoaminika na machafuko nchini humo.