SUDANI-SIASA-USALAMA

Mamia ya wanafunzi wamiminika mitaani dhidi ya utawala wa kijeshi Sudan

Raia wa Sudani wakiandamana mitaani wakati wa maandamano ya kupinga serikali jijini Khartoum, Sudani, Desemba 25, 2018.
Raia wa Sudani wakiandamana mitaani wakati wa maandamano ya kupinga serikali jijini Khartoum, Sudani, Desemba 25, 2018. REUTERS / Mohamed Nureldin Abdallah

Mamia ya wanafunzi wa vyuo vikuu nchini Sudan wameandamana jijini Khartoum wakiimba nyimbo za kuukashifu utawala wa kijeshi, huku wakishinikiza kupatikana haki kwa wanafunzi wenzao waliouawa wakati wa maandamano ya kuuangusha utawala wa rais wa zamani Omar al-Bashir.

Matangazo ya kibiashara

Maanamdano hayo ya wanafunzi yamefanyika ikiwa ni siku chache tu zimepita tangu viongozi wa waandamanaji na Baraza la Kijeshi watie saini mkataba utakaopelekea upatikanaji wa serikali ya mpito.

Maandamano ya jana Jumanne yaliitishwa na shirikisho la wasomi ambalo ndilo lilishiriki kwa kiwango kikubwa kuhamasisha maandamano yaliyomng’oa madarakani rais Bashir.

Baadhi ya wanafunzi waliohojiwa na vyombo vya habari wamesema wengi wa wanafamilia hawataki kulipwa fidia na Serikali yao badala yake wanataka waliohusika wauawe kama walivyouawa wenzao.

Haya yanajiri wakati huu kukiwa na wasiwasi kuhusu utekelezaji wa makubaliano yaliyotiwa saini juma lililopita baada ya baadhi ya makundi ya waasi kuyapinga.