SUDAN-SIASA-USALAMA

Viongozi wa maandamano na washirika wao wafikia makubaliano Sudan

Waandamanaji katika mitaa ya Khartoum, Sudan, Julai 5, 2019.
Waandamanaji katika mitaa ya Khartoum, Sudan, Julai 5, 2019. REUTERS/Mohamed Nureldin Abdallah

Viongozi wa maandamano nchini Sudan pamoja na baadhi ya makundi ya waasi ambao ni washirika wao, wamekubaliana kumaliza tofauti zao kuhusu mkataba wa kugawana madaraka uliotiwa saini kati yao na watawala wa Baraza la Kijeshi, pande hizi zikikubali sasa kufanya kazi pamoja.

Matangazo ya kibiashara

Julai 17 mwaka huu viongozi wa maandamano walitiliana saini na viongozi wa Baraza la Kijeshi, makubaliano ambayo yatapelekea kuundwa kwa utawala wa kiraia baada ya kuangushwa kwa serikali ya Omar al-Bashir.

Haya yanajiri wakati huu wanajeshi wakiripotiwa kuwakamata maofisa kadhaa wa juu wa jeshi wanaotuhumiwa kuhusika katika jaribio la mapinduzi la hivi karibuni.

Shirika rasmi la habari la Sudan SUNA limeripoti kwamba katika jaribio hilo la mapinduzi kundi la maafisa wa jeshi likiongozwa na mkuu wa wafanyakazi, maafisa usalama, viongozi wa harakati za kiislamu na baadhi ya majina kutoka chama kilichokuwa kinatawala walishiriki mapinduzi hayo.

Maafisa takriban 16 wa kijeshi wamekamatwa kufuatia jaribio hilo dhidi ya utawala wa muda unaoshikiliwa na Baraza la Kijeshi nchini Sudan. Luteni Jenerali Gamal Omar ambaye ni mjumbe wa Baraza Kuu la Kijeshi linaloshikilia madaraka katika nchi hiyo amesema vikosi vya usalama vinaendelea hivi sasa kuwasaka maafisa wengine zaidi walioshiriki kwenye njama hiyo ya kutaka kufanya mapinduzi ya kijeshi wiki moja iliyopita.