DRC-USALAMA

DRC: Wafanyakazi wa kampuni ya Canada Banro Mining watekwa nyara Kivu Kusini

Wafanyikazi wa kampuni ya Banro, wanaofanya kazi kwenye mgodi wa Namoya, wametekwa nyara (picha kumbukumbu)
Wafanyikazi wa kampuni ya Banro, wanaofanya kazi kwenye mgodi wa Namoya, wametekwa nyara (picha kumbukumbu) © Banro Corporation

Wafanyakazi wa kampuni ya madini ya Canada Banro Mining hawajulikani waliko baada ya kutekwa nyara Ijumaa, Julai 26 kwenye mgodi wa Namoya, katika mkoa wa Kivu Kusini, kwa mujibu wa maafisa wa mkoa huo.

Matangazo ya kibiashara

Hata hivyo kundi la Mai-Mai Malaika linanyooshewa kidole luwa linahusika na utekaji nyara huo.

Utekaji nyara huo uliotokea katika kijiji cha Matongo, kilomita 7 kutoka mji wa madini wa Salamabila, katika wilaya ya Kabambare katika Jimbo la Maniema, umehusishwa watu wenye silaha wanaotambuliwa kama wanamgambo wa Mai Mai Malaïka, Kundi linaloongozwa na kiongozi wa kivita Sheik Hassan Huzaifa Mitende, ambaye ngome yake kuu inapatikana kusini mwa Mkoa wa Maniema.

Msemaji wa polisi katika eneo hilo Dieudonné Kasereka amesema jeshi la DRC, FARDC, limewakamata washukiwa watatu walioandaa kitendo hicho dhidi ya wafanyakazi wa kampuni ya Banro kutoka Canada. Amebaini kwamba watuhumiwa hao watatu wamekamatwa wakiwasiliana na makundi ya wateka nyara katika msituni. Wanashukiwa kuwa na ukaribu na kundi hilo, amesema Dieudonné Kasereka, huku akiongeza kwamba vikosi vya usalama vimetumwa kuwatafuta mateka hao. Amebaini kwamba mpaka sasa hakuna fidia ambayo imetolewa kwa watekaji nyara.

Mnamo mwezi Machi 2017, wafanyikazi watano, ikiwa ni pamoja na Mfaransa mmoja, walitekwa nyara kabla ya kuachiliwa miezi miwili baadaye.

Mwisho mwa mwezi Juni 2019, kampuni ya Madini ya Namoya ilitaarifu gavana wa Maniema, Augustin Musafiri, juu ya suala la usalama ambao umekuwa hatarini katika neo la Salamabila na kuomba usalama kuimarishwa kwa wafanyikazi wake na kiwanda chake, ambacho pia kilisitisha shughuli zake kwa kipindi cha takriban miezi minne, mwishoni mwa mwaka 2018, kufuatia mdororo wa usalama, na kutishia kusitisha shughuli zake moja kwa moja.