SUDANI-SIASA-USALAMA

Mzozo wa Sudan: Mazungumzo ya mwisho kuanza Jumanne

Mazungumzo ya kutafutia ufumbuzi masuala yaliyobaki kati ya viongozi wa waandamanaji na utawala wa kijeshi nchini Sudan yanatarajiwa Jumanne wiki hii.

Umati wa waandamanaji wakimiminika katika mitaa ya Khartoum, 5udan Julai 2019.
Umati wa waandamanaji wakimiminika katika mitaa ya Khartoum, 5udan Julai 2019. REUTERS/Mohamed Nureldin Abdallah
Matangazo ya kibiashara

Baraza la kijeshi na viongozi wa maandamano tayari wamesaini makubaliano ya kugawana madaraka ambayo yanalenga kuunda baraza tawala la pamoja la kijeshi na kiraia ambalo kisha litapisha utawala wa kiraia

Mazungumzo hayo yatahusu masuala kama vile mamlaka ya baraza tawala liitakaloundwa, kutumika kwa vikosi vya usalama na kinga ya majenerali kutokana na machafuko yanayohusiana na maandamano.

Pande zote mbili zimealikwa kushiriki mazungumzo ya mwisho kuhusu tamko la kikatiba, mpatanishi wa Umoja wa Afrika, Mohamed El Hacen Lebatt, amesema katika taarifa.

Hayo yanajiri wakati waandamanaji kadhaa wakimiminika mitaani mjini Khartoum kuitisha uchuguzi huru kuhusiana na ukandamizaji mkubwa uliofanywa dhidi ya kambi ya maandamano mwezi Juni.

Mapema wiki iliyopita viongozi wa maandamano nchini Sudan na washirika wao wa upande wa makundi ya waasi walifikia makubaliano ya kumaliza tofauti kuhusu makubaliano ya kugawana madaraka na watawala wa kijeshi nchini Sudan.

Mnamo Julai 17 chombo kinachowakilisha vuguvugu la maandamano nchini Sudan kilitia saini makubaliano ya kugawana madaraka na watawala wa kijeshi ambayo yanaweka utaratibu wa kuundwa utawala wa mpito wa kiraia kufuatia kuondolewa madarakani kwa kiongozi wa muda mrefu Omar al-Bashir.

Lakini makundi matatu ya wapaganaji wenye silaha ambao ni sehemu ya vuguvugu la maandamano nchini humo yalipinga makubaliano hayo yakisema yameshindwa kutoa majibu kuhusu mizozo inayoendelea katika majimbo ya Darfur, Kordofan Kusini na Blue Nile.

Kutokana na tofauti hizo kundi la viongozi wa maandamano lilisafiri hadi mji mkuu wa Ethiopia, Addis Ababa, kwa mazungumzo na makundi ya waasi na baada ya siku kadhaa za majadiliano makali walifikia makubaliano ambayo yalitangazwa siku ya Alhamisi wiki iliyopita.