Waandamanaji watano wakiwemo wanafunzi wauawa Al-Obeid
Waandamanaji watano, ikiwa ni pamoja na wanafunzi wanne, wamepigwa risasi leo Jumatatu katika maandamano ya kwanza nchini Sudan siku moja kabla ya kuanza tena kwa mazungumzo kati ya utawala wa kijeshi na viongozi wa maandamano katika kuhitimisha makubaliano kuhusu uongozi wa mpito.
Imechapishwa:
Mazungumzo ya kutafutia ufumbuzi masuala yaliyobaki kati ya viongozi wa waandamanaji na utawala wa kijeshi nchini Sudan yanatarajiwa Jumanne wiki hii.
Sudan, nchi masikini, inayokabiliwa na mdororo wa uchumi, inaendelea kukabiliwa na wimbi la maandamano tangu Desemba 2018. Maandamano ambayo yaliibuka baada ya bei ya mkate kupanda maradufu.
Maandamano hayo yaligeuka na kuwa maandamano dhidi ya serikali ambayo yalisababisha jeshi kumtimuwa na kumkamata rais wa nchi hiyo Omar Hassan Al-Bashir Aprili 11.
Bw Bashir alikuwa madarakani kwa kipindi cha miaka thelathini.
Maandamano yaliendelea baada ya rais kutimuliwa na kuanzishwa kwa Baraza la kijeshi ambalo lilichukuwa mikoba ya Bw. Bashir. Waandamanaji wamekuwa wakiomba utawala wa kiraia na hali bora ya maisha.
Jumatatu wiki hii katika mji wa Al-Obeid, mji mkuu wa Jimbo la Kordofan Kaskazini (katikati mwa nchi), waandamanaji watano wamepigwa risasi katika maandamano ya amani, kwa mujibu wa jopo la madaktari wanao unga mkono waandamanaji.
"Mashujaa watano wameuawa kwa kupigwa risasi na vikosi vya usalama vya serikali wakati walikuwa wakishirikia katika maandamano ya amani," jopo hilo limebaini na kisema kuwa watu kadhaa wamejeruhiwa.