MSUMBIJI-RENAMO-SIASA

Msumbiji: Chama cha RENAMO chasaini mkataba wa amani

Rais wa Msumbiji Filipe Nyusi na kiongozi wa Renamo Ossufo Momade wakumbatiana baada ya kusainiwa kwa mkataba wa mwisho wa amani Agosti 6, 2019 Maputo.
Rais wa Msumbiji Filipe Nyusi na kiongozi wa Renamo Ossufo Momade wakumbatiana baada ya kusainiwa kwa mkataba wa mwisho wa amani Agosti 6, 2019 Maputo. STRINGER / AFP

Serikali ya Msumbuji na waasi wa Renamo wamemaliza mchakato wa muda mrefu kutia saini mkataba wa amani unaolenga kumaliza vita vya muda mrefu.

Matangazo ya kibiashara

Jumanne wiki hii rais Filipe Nyusi na kiongozi wa Renamo Ossufo Momade walitia siani mkataba huo mbele ya wageni mashuhuri na marais wa nchi jirani jijini Maputo, na kuapa kutorudi tena kwenye mapambano.

Umoja wa Mataifa umeelezea hatua hii kama ya kihistoria itakayoleta amani ya kudumu nchini humo.

Kundi la waasi la zamani la RENAMO, ambalo kwa sasa ni chama kikuu cha upinzani nchini Msumbiji tangu mwaka 1990, kilirudi kushika silaha mnamo mwaka 2013 kwa madai ya kugawana madaraka sawa. Tangu kupata uhuru mnamo 1975, Msumbiji imeendelea kutawaliwa na chama cha FRELIMO, chama cha kihistoria cha Samora Machel. Mkataba huo ni jaribio la tatu la kumaliza amani ya kudumu kati ya mahasimu hao wawili. Hatu hiyo inakuja ikiwa imesalia miezi michache kabla ya uchaguzi mkuu, uliopangwa kufanyika mwezi Oktoba mwaka huu. Alhamisi, Agosti 1, Filipe Nyusi na Ossufo Momade walisaini mkataba wa kusitisha uhasama.

Mbele ya marafiki zake marais wa Afrika Kusini na Rwanda, rais wa Msumbiji Filipe Nyusi aliahidi kuimarisha amani ya kudumu.

"Huu sio mkataba kati ya maadui, lakini mkataba ambao unathibitisha kuwa hatutaki vita kati yetu tena. Tunaweza kuwa na tofauti, kama familia moja, lakini mazungumzo ndio yatakuja kutatatua tofauti zetu. Kamwe matokeo ya uchaguzi hayatatatiza amani.

Na kuhusu uchaguzi, kulikuwa na mazungumzo mengi wakati wa kutiwa saini kwa mkataba huo. Uchaguzi Mkuu unatarajiwa kufanyika Oktoba 15. Uchaguzi huo ni mtihani muhimu kwa nchi yenye rasilimali nyingi za madini pamoja na visma vya gesi zenye thamani. "Kwa hivyo uchaguzi wenye amani ni muhimu kwa nchi yetu, amesema Ossufo Momade, Kiongozi wa chama cha RENAMO. "Tutapitia upya wito wetu wa kutofanya makosa kama zamani na kuandaa mazingira mazuri ya kufanyikakwa uchaguzi huru, wa haki na wa wazi, na kwamba umwagaji damu hauana nafasi tena, " ameingeza kiongozi wa chama cha RENAMO.

Lakini kwa upande wa Baltazar Fael, mpelelezi wa Kituo cha Uadilifu wa Umma nchini Msumbiji, anasema mkataba huo umeharakishwa ili kuruhusu kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu Oktoba 15, lakini hautafutii ufumbuzi kwa kina matatizo yanayolikabili taifa hilo. "Swali hili la amani limekuwa mafanikio makubwa katika kipindi cha kwanza cha Filipe Nyusi. Nadhani mkataba huu hauko wazi kwa njia nyingi. Filipe Nyusi aliishinikiza chama cha RENAMO ili wakamilishe mazungumzo yao. Lakini ikiwa tutaangalia kwa karibu, hata swali la DDR, kuwarejesha maisha ya kiraia wapiganaji, hatujui itakuwaje mwisho, ikiwa RENAMO itaweka nchini silaha zake zote, au ikiwa bado ina wasiwasi na serikali na mwishowe kuamua kubaki na silaha. Kwa sababu ngao yake kubwa ni silaha hizo inazomiliki kwa kushinikiza serikali kukubali kushiriki mazungumzo. Kwa hivyo ikiwa Renamo itajisalimisha na kukabidhi silaha katika mazingira haya ya kutoaminiana, itakuwa mwisho wa chama hicho, " amesema Baltazar Fael.

Wapiganaji 5,200 wa Renamo sasa wanatakiwa kukabidhi silaha zao kwa serikali ya Msumbiji.