DRC-EBOLA-WHO-USALAMA

Madaktari watatu wakamatwa kwa kuhusika na mauaji ya daktari mwenzao Butembo

Wafanyakazi wa kitengo cha matibabu katika kituo cha matibabu cha Ebola Machi 9, 2019 Butembo, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Wafanyakazi wa kitengo cha matibabu katika kituo cha matibabu cha Ebola Machi 9, 2019 Butembo, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo. AFP

Madaktari watatu nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, wanashikiliwa na maafisa wa usalama, baada ya kuhusishwa na kifo cha Daktari wa Shirika la Afya Duniani (WHO), aliyekuwa anatoa tiba kwa wagonjwa wa Ebola.

Matangazo ya kibiashara

Kiongozi wa mashtaka wa kijeshi amethibitisha hilo, baada ya kubainika kuwa Daktari huyo Richard Valery Mouzoko Kiboung raia wa Cameroon, aliuawa kwa kupigwa risasi mwezi Aprili baada ya watu wenye silaha kushambulia hospitalini mjini Butembo.

Madaktari wanaozuiwa watafunguliwa mashtaka ya ugaidi na upangaji wa uhalifu, baada ya maafisa wa usalama kusema kuwa walikuwa na ushahidi unaonesha kuwa madktar hao wa DRC walikutana na kupanga kuuawa kwa Daktari huyo wa WHO.

Daktari Mouzoko ni miongoni mwa maafisa wa afya waliotumwa na shirika la Afya Duniani (WHO) katika mkoa wa Kivu Kaskazini, kusaidia kutoa matibabu kwa wagojwa wa Ebola tangu mwaka 2018, ugonjwa ambao umesababisha watu zaidi ya 1,800 kupoteza maisha hadi sasa.

Hata hivyo, kukamatwa kwa Madakatri hao kumezua hasira miongoni mwa Madaktari mjini Butembo ambao wametishia kugoma iwapo wenzao hawataachiliwa huru baada ya saa 48.