AFRIKA KUSINI-USALAMA

Chuki dhidi ya raia wa kigeni yaendelea Afrika Kusini

Afisa wa polisi akikabiliana na wezi ambao wanataka kushambulia duka linalomilikiwa na raia wa kigeni katika eneo la Turffontein, Johannesburg. Septemba 2, 2019.
Afisa wa polisi akikabiliana na wezi ambao wanataka kushambulia duka linalomilikiwa na raia wa kigeni katika eneo la Turffontein, Johannesburg. Septemba 2, 2019. © Michele Spatari / AFP

Raia wa kigeni nchini Afrika Kusini wanaendelea kukumbwa na visa mbalimbali hasa kuuawa, mali zao kuchomwa na madhila mengine. Baadhi ya raia wa Afrika Kusini wenye itikadi kali za kikabila wananyooshewa kidole cha lawama kwa kuhusika na vitendo hivyo.

Matangazo ya kibiashara

Maduka mengi yanayomilikiwa na raia wa kigeni yameendelea kuchomwa moto tangu Jumapili Septemba 1, na watu watatu wameuawa katika machafuko hayo mjini Johannesburg kwa mujibu wa mamlaka katika mji huo.

Maandamano dhidi ya raia wa kigeni yanaendelea katika nchi hiyo, maandamano ambayo yalizinduliwa na madereva wa malori, ambao wamekuwa wakiwakamata madereva wa kigeni kwa wiki kadhaa na kuchoma moto mizigo wanayosafirisha. Maandamano hayo yaliongezeka wiki iliyopita katikati mwa mji mkuu wa Pretoria, kumekuwa na visa vya uporaji katika maduka mengi ya wahamiaji.

Baadhi ya raia wa kigeni wanasema maandamano hayo yalizinduliwa na mashirika kadhaa yanayotambuliwa serikalini. Miongoni mwa mashirika hayo ni pamoja na madereva wa lori na vyama vya madereva wa teksi. Kama wiki iliyopita katika mji wa Pretoria, madereva wa teksi katika mji wa Johannesburg walchoma maduka kadhaa yanayomilikiwa na raia wa kigeni.

Ukatili huu sio wa hivi sasa. Mwaka mmoja uliopita, madereva wa kigeni, raia wa Zimbabwe, DRC au Zambia waliteswa barabarani wakishtumiwa kuwaibia kazi wenyeji. Watu 200 wameuawa katika vurugu hizo kwa kipindi cha mwaka mmoja nchini Afrika Kusini.