ZIMBABWE-MUGABE-SIASA

Mwili wa Robert Mugabe wasafirishwa kutoka Singapore kwenda Zimbabwe

Rais wa zamani wa Zimbabwe Robert Gabriel Mugabe, Oktoba 3, 2017.
Rais wa zamani wa Zimbabwe Robert Gabriel Mugabe, Oktoba 3, 2017. Phill Magakoe / AFP

Mwili wa rais wa zamani wa Zimbabwe Robert Gabriel Mugabe umeondoka Singapore mapema leo Jumatano asubuhi kwenda nchini Zimbabwe ambapo atazikwa baada ya maombolezo ya kitaifa, mpwa wake Adam Molai ametangaza.

Matangazo ya kibiashara

Robert Gabriel Mugabe alifariki dunia Septemba 6 akiwa na umri wa miaka 95 nchini Singapore, ambapo alikuwa akihudumiwa kimatibabu kwa miezi zaidi ya mitano.

Rais wa zamani wa Zimbabwe anatarajiwa kuzikwa Jumapili, Septemba 15 baada ya sherehe rasmi ambayo itafanyika Jumamosi. Hata hivyo familia ya Zimbabwe haijakubaliana na serikali sehemu ambapo atazikwa kiongozi huyo wa zamani wa Zimbabwe.

Tangu Ijumaa, Rais Emmerson Mnangagwa ametangaza maombolezo ya kitaifa na kumpa mtangulizi wake hadhi ya "shujaa wa kitaifa", ambayo inampa nafasi kuzikwa katika "makaburi ya Mashujaa wa Taifa". Lakini familia ya rais haijajapendelea kiongozi wao kuzikwa katika makaburi hayo.

Mishoni mwa wiki iliyopita mpwa wa Mugabe, Leo Mugabe alisema hajui ni wapi mjomba wake alitaka kuzikwa. Lakini mazishi katika "makaburi ya Mashujaa wa Taifa", kama ilivyopangwa kabla ya kutimuliwa kwake madarakani, yatakuwa mazishi rasmi yaliyoandaliwa na aliyemuangusha Robert Mugabe, Emmerson Mnangagwa. Jambo ambalo litaleta shida kwa familia, aliongeza Leo Mugabe.

Katika makaburi hayo ndipo alizikwa mke wa kwanza wa Robert Gabriel Mugabe, Sally. Eneo ambalo lilijengwa kwa msaada wa Korea Kaskazini.

Sally, alikuwa mmoja wa wanaharakati wa ukombozi wa Zimbabwe, aliyetazamwa na wengi hadi kifo chake kama mama wa taifa la Zimbabwe.

Historia ya maisha na siasa za Robert Mugabe

Robert Mugabe alizaliwa mwezi Februari mwaka 1924, katika familia ya Kikristo ya Katoliki katika eneo la Kutama, Kaskazini Magharibi mwa jiji kuu Harare, wakati huo Zimbabwe ikifahamika kama Southern Rhodesia.

Waliomfahamu vema akiwa mtoto, wanasema alipenda sana kusoma vitabu hata wakati alipokuwa anachunga mifugo msituni.

Miaka ya sitini, alianza harakati za kupigania nchi yake kuwa huru kutoka mikononi kwa Wazungu wachache kutoka nchini Uingereza waliokuwa wanatawala taifa lenye idadi kubwa ya Waafrika.

Harakati zake za kutaka waafrika kujiongoza na kumiliki ardhi, zilisababisha akafungwa jela miaka 10 na serikali ya wakoloni kati ya mwaka 1964 hadi 1974.

Baada ya kuachiliwa huru, alikimbilia nchini Msumbiji na kuunda vuguvugu la ZANU PF kuanizisha vita vya msituni kupambana na serikali ya kikoloni, wakati huo ikiongozwa na Waziri Mkuu Ian Smith.

Wakati huo wa mapambano ya msituni, serikali ya Uingereza ilianzisha mchakato wa mazungumzo na vuguvugu hilo, na kupelekea usitishwaji wa mapigano na Uchaguzi ukafanyika mwaka 1980.

ZANU PF kilishinda Uchaguzi huo na Mugabe kuwa Waziri Mkuu wa kwanza mweusi nchini Southern Rhodesia ambayo ilibadilishwa njia na kuitwa Zimbabwe.

Baadaye, wadhifa wa Waziri Mkuu uliondolewa na Mugabe akawa rais wa nchi hiyo kwa zaidi ya miaka 30 hadi alipolazimishwa kuondoka madarakani na jeshi mwezi Novemba mwaka 2017.

Wengi watamkumbuka Mugabe kama mpiganiaji huru wa Zimbabwe na kiongozi ambaye alipigania umoja wa bara la Afrika na kuwasaidia wananchi wa taifa lake kupata mashamba na elimu.

Hata hivyo, kuna wale watakaomkumbuka kama dikteta, aliyekiuka haki za binadamu na kuminya demokrasia.