DRC-UBELGIJI-USHIRIKIANO

Ziara ya Tshisekedi Ubelgiji yaibua maswali mengi

Félix Tshisekedi atia saini kitabu cha dhahabu cha wageni wa heshima cha Mfalme wa Ubelgiji Philippe wakati wa ziara yake ya kiserikali, Septemba 17, 2019.
Félix Tshisekedi atia saini kitabu cha dhahabu cha wageni wa heshima cha Mfalme wa Ubelgiji Philippe wakati wa ziara yake ya kiserikali, Septemba 17, 2019. © REUTERS/Francois Lenoir

Ziara ya kiserikali ya Rais wa DRC Felix Tshisekedi Tshilombo nchini Ubelgiji imeendelea Jumanne hii Septemba 17. Lakini mapokezi ya Rais wa DRC kwa viongozi wa Brussels yameibua maswali mengi, ikiwa ndani na nje ya nchi.

Matangazo ya kibiashara

Nchi hizo mbili zimesaini nakala kadhaa kuashiria kuanza tena kwa ushirikiano kabla ya Felix Tshisekedi kupokelewa na Mfalme wa Ubelgiji. Lakini ziara hii yenye lengo la kufufua ushirikiano na kuboresha uhusiano kati ya DRC na Ubelgiji haikuwafurahisha raia wote wa DRC, baadhi wamekosoa na wengine wamekaribisha.

Wananchi kadhaa wa DRC walijaribu kuandamana kabla ya kutawanywa na polisi wa Ubelgiji, mbali na maeneo rasmi. Wanalaumu Ubelgiji kwa kumpokea Rais Felix Tshisekedi wakati uchaguzi wake ulipingwa.

"Tuko hapa kuelezea kutoridhishwa kwetu kwa kukaribishwa Bwana Tshisekedi hapa Ubelgiji. Wakongo mnaowaona hapa hawamtambui Bw Tshisekedi kama rais wa DRC. Kwetu sisi, tunaona kuwa alifanya mapinduzi ya uchaguzi nchini DRC, " mmoja kati ya waandamanaji amesem aalipokuwa akihojiwa na mwanahabari wetu Sonia Rolley

Nchini DRC, pia, upinzani umeonyesha kutoridhika na ziara hiyo ya Rais Felix Tshisekedi nchini Ubelgiji. Kwa upande wa Martin Fayulu, mgombea urais aliyeshindwa katika uchaguzi wa urais na ambaye anaendelea kupinga matokeo ya uchaguzi, amesema Ubelgiji imempokea mtu ambaye hana uhalali wa kisiasa.

"Baada ya taarifa zilizotolewa na wanasiasa wa Ubelgiji, nadhani ni ukosefu wa heshima kwa wananchi wa DRC. Wanapokea mtu anayepuuzia demokrasia ? (...) Bwana Félix Tshisekedi hataweza kufanya chochote mwenyewe kwa sababu hana uwezo wa sera yake. Kabila bado yupo, anasubiri na anaongoza kila kitu, " amesema Martin Fayulu, akihojiwa na mwanahabari wetu Coralie Pierret.