DRC-FDLR-RWANDA-USALAMA

DRC: Maswali mengi yaibuka kuhusu kifo cha kiongozi wa FDLR

Waasi wa Kihutu wa Rwanda wa FDLR, kilomita 150 kaskazini mashariki mwa Goma, mwaka 2009.
Waasi wa Kihutu wa Rwanda wa FDLR, kilomita 150 kaskazini mashariki mwa Goma, mwaka 2009. ©AFP/ Lionel Healing

Katikati mwa wiki hii jeshi la Jamhuri ya Kidemkorasia ya Congo (FARDC) lilitangaza kwamba "lilimuua" kiongozi mkuu wa kundi la waasi wa Kihutu wa Rwanda (FDLR), Sylvestre Mudacumura. Maswali mengi yameibuka siku moja tu baada ya kuuawa kwa kiongozi huyo.

Matangazo ya kibiashara

Wengi wanajiuliza nani aliyemuua kiongozi huyo mkuu wa kivita wa kundi la waasi la FDLR? Kwa mujibu wa msemaji wa jeshi la DRC, Jenerali Léon-Richard Kasongo, jeshi la DRC (FARDC) ndilo "limefaulu kumuangamiza kiongozi huyo wa FDLR na ni ushindi kwa jeshi la FARDC".

Lakini mashirika ya kiraia na wakaazi wa mkoa wa Kivu Kaskazini wanahakikisha kuwa wanamgambo wa kundi linaloongozwa na Jenerali Guidon, ambaye anakabiliwa na waranti wa kukamatwa wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu wa Kivita (ICC), waalishiriki katika operesheni ya kuwasaka wapiganaji wa FDLR. Hata hivyo serikali ya Kinshasa imekanusha madai hayo na kubaini kwamba askari wake pekee ndio walioshiriki katika operesheni ya kumuangamiza kiongozi huyo mkuu wa FDLR.

Kwa hatua hii, bado "ni mapema kusema ni nani hasa aliyefanya operesheni hii," Fred Bauma, kutoka taasisi ya kutathmini kuhusu DRC, amesema. "Je! Ni FARDC ndo waliendesha operesheni hii, je! Waliiendesha peke yao? Na ni makundi gani au vikosi gani vingine ambavyo vilishiriki katika operesheni hii?amehoji Fred Bauma.

Swali lingine linahusu mazingira halisi ya kuuawa kwa Sylvestre Mudacumura. Msemaji wa jeshi la DRC alibaini kwamba Sylvestre Mudacumura na maafisa wake waliingiliwa ghafla katika maficho yao kabla ya "kuuawa kabisa", bila hata hivyo kutoa maelezo zaidi.

Jean-Robert Senga, mtafiti kuhusu DRC kwa niaba ya shirika la kimtaifa la Haki za Binadamu la Amnesty International, amesema ni "muhimu kwa jeshi la FARDC kueleza mazingira ya kifo cha Sylvestre Mudacumura," akibaini kwamba ushahidi wanao ni kwamba kiongozi huyo wa FDLR aliuawa kikatili. " "Angelipaswa kukamatwa na kukabidhiwa ICC kwa ili haki iweze kutendeka," Jean-Robert Senga amesema.

Kifo chake kitakuwa na athari kwa kundi lake, ambalo tayari limedhoofika. Uwezo wa kundi la FDLR umepunguzwa kwa miaka kadhaa sasa, ameongeza Fred Bauma.