COTE D'IVOIRE-ICC-GBAGBO-HAKI

Mawakili waomba marekebisho ya masharti ya Laurent Gbagbo kuachiliwa huru

Rais wa zamani wa Cote d'Ivoire Laurent Gbagbo.
Rais wa zamani wa Cote d'Ivoire Laurent Gbagbo. © AFP/Issouf Sanogo

Mawakili wa Laurent Gbagbo wanajaribu kupata kutoka Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu wa Kivita, ICC, marekebisho ya masharti ya mteja wao kuachiliwa huru.

Matangazo ya kibiashara

Upande wa utetezi wa rais huyo wa zamani wa Cote d'Ivoire unataka masharti yaliyowekwa kwa mteja wao kuachiliwa huru Januari 15 mwaka huu, yaweze kufanyiwa marekebisho. Rais wa zamani wa Cote d'Ivoire, ambaye bado yuko Brussels chini ya usimamizi wa mahakama, hadi sasa hajaruhusiwa na ICC kuondoka mji mkuu wa Ubelgiji.

Licha ya kuachiliwa huru, Laurent Gbagbo amewekwa chini ya usimamizi wa mahakama na hawezi kuondoka nje ya mji mkuu wa Ubelgiji bila idhini ya mahakama. Vivyo hivyo kwa Charles Blé Goudé ambaye bado yuko mjini Hague.

Wawili hao wanapaswa kufutiwa uamuzi wa kuwekewa masharti kwa kuachiliwa kwao.

Laurent Gbagbo amepinga masharti hayo na kubaini kwamba yanamzuia kushiriki uchaguzi wa urais uliopangwa kufanyika mwakani.