DRC-ADF-USALAMA

DRC: Felix Tshisekedi atangaza mashambulizi ya mwisho dhidi ya ADF Beni

Rais wa DRC Félix Tshisekedi (katikati) akihutubia umati wa watu uliokusanyika mbele ya manispaa ya jiji la Beni, Aprili 16, 2019.
Rais wa DRC Félix Tshisekedi (katikati) akihutubia umati wa watu uliokusanyika mbele ya manispaa ya jiji la Beni, Aprili 16, 2019. Luke Dennison / AFP

Katika mkutano aliofanya Alhamisi Oktoba 10 karibu na randabauti Nyamwisi katika mji wa Beni, mkoani wa Kivu Kaskazini, Rais wa DRC Felix Tshisekedi ametangaza kuwa hivi karibuni jeshi la DRC litazindua "mashambulizi ya mwisho dhidi ya kundi la waasi wa Uganda la ADF" ili kurejesha amani katika kanda hiyo.

Matangazo ya kibiashara

"Nitarudi hapa tena wakati mkoa utakuwa cini ya udhibiti kamili wa jeshi la DRC, FARDC, kwa sababu tunakaribia kuzindua mashambulizi ya mwisho dhidi ya wapiganaji wa kundi la ADF katika siku zijazo ili kuwatimuwa kabisa. Mungu awalinde! “, amesema Rais Tshisekedi, akinukuliwa na radio Okapi.

Waasi hao kutoka Uganda wanashtumiwa kuendesha mauaji ya maelfu ya raia katika miaka mitano iliyopita katika kanda hiyo.

Felix Tshisekedi pia ameahidi kufufua kilimo katika kanda hiyo; kabla ya kutangaza kuanza hivi karibuni ujenzi wa barabara zitakazounganisha miji ya Kasindi-Beni-Butembo, Beni-Kisangani na Mbau-Kamango.