Afrika Kusini: Rais wa zamani Jacob Zuma kufikishwa kizimbani kwa rushwa
Imechapishwa:
Rais wa zamani wa Afrika Kusini, Jacob Zuma, anayendelea kukabiliwa na kashfa mbalimbali zilizosababisha kung'atuliwa madarakani mwaka 2018, anatarajiwa kuanza kusikilizwa Jumanne wiki hii kwa mara ya kwanza katika Mahakama Kuu ya Pietermaritzburg kuhusiana na rushwa.
Kesi yake inahusiana na rushwa katika kesi ya zamani, miaka ishirini iliyopita, ya mkataba wa silaha, kesi ambayo inaihusisha kampuni ya Ufaransa Thales.
Jacob Zuma, aliyekaa madarakani kuanzia mwaka 2009 hadi mwaka 2018, anashitakiwa kwa kosa la ufisadi, utakatishaji wa fedha na kupitisha mlango wa nyuma pesa kuhusu mkataba mkubwa wa silaha wa Randi bilioni 51 (sawa na Euro bilioni tatu kwa bei ya sasa) mkataba uliotolewa mwaka 1999.
Wakati wa mashtaka dhidi yake, alikuwa "waziri" katika ngazi ya mkoa na baadaye makamu wa rais. Anatuhumiwa kuwa alipokea Randi milioni 4 ( sawa na Euro 249,000 kwa bei ya sasa) kama hongo kutoka kampuni ya Ufaransa ya Thales.
Jacob Zuma na kampuni hiyo inayotengeneza vifaa vya kielektroniki na ulinzi, ambayo pia inakabiliwa na mashitaka hayo, wameendelea kukana mashitaka dhidi yao.
Baada ya kesi hiyo kusheleweshwa kwa miaka kumi na tano, Mahakama, siku ya Ijumaa ya wiki iliyopita iliamua kuruhusu kesi hiyo inayomkabili rais wa zamani wa Afrika Kusini kuanza kusikilizwa kwa undani, baada ya kufutilia mbali ombi la Jacob Zuma la kuachana na mashtaka dhidi yake.
Kesi hiyo inatarajiwa kuanza leo Jumanne katika Mahakama Kuu ya Pietermaritzburg, Mashariki mwa Afrika Kusini. "Kesi hiyo imepangwa kuanza kusikilizwa" Jumanne wiki hii, msemaji wa ofisi ya mashitaka Natasha Kara amelithibitisha shirika la habari la AFP.