UFARANSA-MALI-GSIM-USALAMA

Waziri wa Jeshi atangaza kifo cha kiongozi wa kijihadi nchini Mali

Morogan Abou Abderahman al Maghrebi, kwa jina maarufu Ali Maychou, anayechukuliwa kama kiongozi namba mbili wa kidini wa kundi la wanamgambo la GSIM, kundi lenye mafungamano na Al Qaeda, aliuawa na vikosi vya Ufaransa nchini Mali mapema mwezi Oktoba, Waziri wa Jeshi, Florence Parly amesema.

VPS, gari ya doria Maalum inayotumiwa na vikosi vya Ufaransa karibu na Timbuktu nchini Mali.
VPS, gari ya doria Maalum inayotumiwa na vikosi vya Ufaransa karibu na Timbuktu nchini Mali. RFI/ OLivier Fourt
Matangazo ya kibiashara

Waziri Florence Parly amethibitisha kifo hicho alipokuwa akirudi katika ndege kutoka katika eneo la Sahel, ambapo alitoa matangazo mengi na kulithibitisha shirika la Habari la AFP.

Kiongozi mkuu wa kijihadi aliuawa "usiku wa tarehe 8 kuamkia tarehe 9 Oktoba" nchini Mali kwa ushirikiano na vikosi vya Mali na msaada kutoka Marekani, Waziei wa Jeshi wa Ufaransa amesema.

Ali Maychou alikuwa "kiongozi namba mbili wa kigaidi aliyekuwa akisakwa katika ukanda wa Sahel n anchi kadhaa ikiwa ni pamoja na Marekani," Waziri Florence Parly ameongeza.

Ali Maychou alijiunga na kundi la Al-Qaeda katika ukanda wa Maghreb (Aqmi) mnamo mwaka 2012. Akawa kiongozi wa kiroho kabla ya kushiriki katika uundwaji wa kundi la wanamgambo wa Kiislamu la GSIM mnamo mwaka 2017 akishirikiana na Iyad ag Ghali, namba moja wa kundi hilo, ambaye alikuwa mshirika wake wa karibu.

Kundi la GSIM lilidai kuhusika na mashambulizi ya hivi karibuni mwishoni mwa mwezi Septemba na mapema mwezi Oktoba dhidi ya vikosi vya Mali katika miji ya Boulkessi na Mondoro ambapo askari 40 waliuawa. Kundi hilo pia lilidai kuhusika na shambulio katika mji mkuu wa Burkina Faso, Ouagadougou mwamo mwezi Machi 2018, ambapo watu 8 waliuawa). Mashambulizi ya Ouagadougou ya mwaka 2016 yaliua watu 30 na mwaka 2017 mashambulizi mengine yaliua watu 19). Mashambulizi yote hayo yalitekelezwa na kundi la Al Qaeda.