UFARANSA-DRC-USHIRIKIANO

Ufaransa yakubali kutoa msaada wa Euro milioni 65 kwa DRC

Emmanuel Macron na Félix Tshisekedi katika ikulu ya Elysée, Novemba 12, 2019.
Emmanuel Macron na Félix Tshisekedi katika ikulu ya Elysée, Novemba 12, 2019. © REUTERS/Johanna Geron

Kufuatia mkutano na mwenzake wa DRC Felix Tshisekedi, Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron ametangaza kwamba Ufaransa itaitolea DRC msaada wa Euro milioni 65 katika mkataba wa maendeleo na kupunguza madeni yanayoikabili nchi hiyo.

Matangazo ya kibiashara

Paris itasaidia katika miradi ya marekebisho na mabadiliko iliyoanzishwa na Felix Tshisekedi, Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron ametangaza.

Ufaransa itasaidia kwanza nchi ya DRC kutokomeza makundi yenye silaha, haswa Mashariki mwa nchi hiyo. Ushirikiano utajikita katika masuala ya kupeana taarifa (upelelezi), lakini pia katika masuala ya kijeshi. Paris pia inatarajia kuchukua hatua za kidiplomasia kwenye Umoja wa Mataifa, kwa kuwaadhibu viongozi wa makundi hayo yenye silaha. Katika suala hili la usalama, Rais Emmanuel Macron amesema ana matumaini kwamba nchi zote za ukanda zitajitolea kushirikiana na rais wa DRC, haswa Rwanda na Uganda.

Ufaransa pia itaitolea DRC msaada katika sekta ya elimu. Milioni ishirini na tatu zitatolewa ili kusaidia mradi wa elimu ya bure. Paris itajikita haswa kwa kuwatolea mafuzo waalimu. Ufaransa pia itaendelea kusaidia nchi hiyo kwa maswala ya afya. "Kurejesha utulivu, kurejelea upya mfumo wa afya katika mikoa yote kwa kumuunga mkono Rais Tshisekedi ni hatua muhimu sana kwetu," amesema Emmanuel Macron. Rais wa Ufaransa amehakikishia kwamba Ufaransa itaongeza jitihada na kuchukuwa hatua katika nyanja zingine nyingi kama vile kilimo, mazingira au kuendeleza lugha ya Kifaransa nchini humo.

Rais Tshisekedi, kwa upande wake, amekaribisha Ufaransa kuona "inarudi kusaidia katika skta zote hizo."

Rais wa DRC anataraji kurudi nchini Ufaransa mwezi Juni mwakani kwa mkutano wa kilele kati ya Afrika na Ufaransa.

Emmanuel Macron amekubali mwaliko wa Félix Tshisekedi. Atazuru DRC mwaka ujao.