CHANJO-EBOLA-DRC-RWANDA

Chanjo ya pili dhidi ya Ebola yaanza kutolewa nchini DRC na Rwanda

Kituo cha kutoa chanjo ya Ebola mjini Goma
Kituo cha kutoa chanjo ya Ebola mjini Goma REUTERS/Baz Ratner/File Photo

Serikali ya Rwanda na DRC zimezindua kampeni ya utoaji chanjo ya Ebola ya Johson and Johnson kwenye mji wa Rubavu kwa lengo la kupambana na maambukizi ya ugonjwa hatari wa Ebola.

Matangazo ya kibiashara

Shirika la WHO limesema kwamba Raia wasiopungua 200,000  wilayani Rubavu na Rusizi ndio watakaopewa chanjo hiyo na maelfu mjini Goma.

Ibrahim Soce mwakilishi wa WHO nchini humo, amesema, hatua hiyo ni muhimu sana katika vita dhidi ya Ebola.

“Tunawashukuru viongozi wa DRC na Rwanda ambao kwa pamoja wameendelea kuunga mkono mapambano dhidi ya Ebola katika nchi zao,” alisema.

Chanjo hii inaanza kutolewa kutokana na ushauri wa Shirika la Afya Duniani WHO ambapo imezitaka nchi zote zilizoko hatarini kupata maambukizi ya Ebola kutumia chanjo hiyo.

Daktari Sabin Nsanzimana, mkurugenzi wa kituo cha magonjwa ya mlipuko nchini Rwanda amesema chanjo hiyo itasaidia pakubwa katika maambukizi mapya ya ugonjwa huo hatari.

Tangu kuzuka kwa ugonjwa huu mashariki mwa DRC, watu zaidi ya 1,800 wameripotiwa kupoteza maisha, huku nchi jirani zikitajwa kuwa kwenye hatari ya kupata maambukizi ikiwa hazitachukua tahadhari.