DRC-EU-VIKWAZO

Umoja wa Ulaya waondoa vikwazo dhidi ya maafisa wawili wa DRC

Waziri wa zamani wa habari DRC, Lambert Mende.
Waziri wa zamani wa habari DRC, Lambert Mende. © FEDERICO SCOPPA / AFP

Mawaziri wa Mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya wanakutana tangu Jumatatu hii asubuhi Desemba 9 jijini Brussels. Miongoni mwa mada zilizojadiliwa, ni pamoja na uhusiano wa umoja huo na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Matangazo ya kibiashara

Katika kikao hicho pia wamejadili kuhusu orodha ya maafisa wa DRC wanaokabiliwa na vikwazo vya Umoja wa Ulaya. Hata hivyo maafisa wawili wa nchi hiyo wameondolewa kwenye orodha hiyo.

 

Walioondolewa vikwazo ni pamoja na waziri wa zamani wa habari Lambert Mende, na mkuu wa kitengo cha Usalama wa taifa Roger Kibelisa.

Waliwekwa kwenye orodha ya maafisa waliochukuliwa vikwazo na Umoja wa Ulaya kwa "kutatiza suluhisho la amani na makubaliano" kwa minajili ya uchaguzi nchiniJamhuri ya Kidemokrasia ya Congo. Tangu wakati huo, uchaguzi ulifanyika na Umoja wa Ulaya umeamua kwamba hakuna sababu ya kuendelea kuweka vikwazo dhidi ya maafisa hao kwa kile umoja huo umeita "hatua za kushinikiza".

Hata hivyo Umoja wa Ulaya umeongeza muda wa mwaka mmoja zaidi wa vikwazo dhidi ya maofisa 12 waliokuwa chini ya utawala wa aliyekuwa rais wa DRC, Joseph Kabila Kabange. miongoni mwa maafisa hao ni pamoja na waziri wa zamani wa mambo ya ndani Evariste Boshab, mkuu wa zamani wa polisi jijini Kinshasa, Celestin Kanyama, na mgombea urais wa zamani Ramazani Shadari.

Umoja wa Ulaya pia umetangaza kusaidia hatua kwa hatua mpango wa mageuzi ya serikali ya DRC. Kwa upande wa umoja wa wa Ulaya, zoezi la kupishana kwenye madaraka kwa amani ambalo ni la kwanza katika historia ya nchi hiyo limefungua "fursa ya utulivu na maendeleo ya umoja nchini DRC na katika ukanda mzima".

■ Orodha ya maafisa wa DRC ambao wanaendelea kukabiliwa na vikwazo vya Umoja wa Ulaya: Ilunga Kampete - Gabriel Amisi Kumba - Ferdinand Ilunga Luyoyo - Celestin Kanyama - John Numbi - Delphin Kahimbi - Evariste Boshab - Alex Kande Mupompa - Jean-Claude Kazembe Musonda - Éric Ruhorimbere - Emmanuel Ramazani Shadari - Kalev Mutondo