LIBYA-USALAMA

Jumuiya ya nchi za Kiarabu zapinga suala la kuingilia kijeshi Libya

Wawakilishi wa kudumu wa Jumuiya ya nchi za Kiarabu wanashiriki katika mkutano wa dharura kujadili mipango ya Uturuki ya kupeleka wanajeshi nchini Libya katika makao makuu ya jumuiya hiyo Cairo, Misri, Desemba 31, 2019.
Wawakilishi wa kudumu wa Jumuiya ya nchi za Kiarabu wanashiriki katika mkutano wa dharura kujadili mipango ya Uturuki ya kupeleka wanajeshi nchini Libya katika makao makuu ya jumuiya hiyo Cairo, Misri, Desemba 31, 2019. REUTERS/Mohamed Abd El Ghany

Katika mkutano maalumu uliofanyika Jumanne jijini Cairo, Jumuiya ya nchi za Kiarabu imesisitiza juu ya umuhimu wa kuzuia nchi yoyote kuingilia katika masuala ya Libya.

Matangazo ya kibiashara

Mkutano huu, wa kwanza wa Jumuiya ya nchi za Kiarabu kuhusu Libya tangu 2011, ulifanyika kwa ombi la Misri.

Mkutano huu umefanyika wakati Uturuki inajiandaa kutuma wanajeshi wake nchini Libya. Ushahidi unaendelea kutolewa kuhusu Uturuki kutuma wapiganaji wa Syria wanayoiunga mkono kusaidi serikali ya Tripoli inayotambuliwa na jumuiya ya kimataifa.

Azimio lililopitishwa mwishoni mwa mkutano huu wa dharura unapinga nchi yoyote kuingilia katika masuala ya Libya, hali "ambayo inaweza kusaidia kuwezesha wapiganaji wa kigaidi wenye itikadi kali kutoka nchi za kigeni kuingia nchini Libya".

Wajumbe wa kudumu wa Jumuiya ya nchi za Kiarabu pia wameelezea wasiwasi wao kuhusu nchi zao kwa kuongezeka kwa mapigano ambayo "yanazidisha hali mbaya nchini Libya" na "yanatishia usalama na utulivu wa nchi jirani katika ukanda wote", kwa mujibu wa wajumbe hao.

Wiki iliyopita, kufuatia ziara ya kushtukiza ya Recep Tayyip Erdogan nchini Tunisia, Rais Kaïs Saïed alilazimika kukanusha taarifa ya mwenzake wa Uturuki ambaye alisema kwamba Tunis ilikubaliana na Ankara kusaidia serikali ya Fayez el-Sarraj.

Algeria, ambayo pia ilipata shinikizo kutoka Uturuki, imetangaza kwamba haitaungana na Uturuki kusaidia serikali ya Tripoli na kwamba inapinga nchi yoyote kuingilia kijeshi nchini Libya.