LIBYA-MISRI-UTURUKI-USALAMA

Uturuki kuingilia kijeshi Libya: Rais wa Misri afutilia mbali hatua ya bunge la Uturuki

Rais Abdel Fattah al-Sissi (picha ya kumbukumbu).
Rais Abdel Fattah al-Sissi (picha ya kumbukumbu). AFP/Egyptian Presidency/Str

Rais wa Misri Abdel Fattah al-Sisi amesema nchi yake haitokubali nchi yoyote kuingia kijeshi nchi ya Libya kusaidia upande wowote. Libya inaendelea kukumbwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Matangazo ya kibiashara

Kauli inakuja baada ya Bunge la Uturuki kupitisha azimio la serikali la kutuma askari nchini Libya kusaidai serikali ya kitaifa ya Tripoli inayotambuliwa na jumuiya ya kimataifa.

Alhamisi wiki hii rais wa Misri Abdel Fattah al-Sisi aliitisha mkutano wa dharura wa Baraza la Usalama la Kitaifa, mkutano uliojumuisha Waziri wa Ulinzi, Waziri wa Mambo ya Ndani, Waziri wa Mambo ya nje na mkuu waidara ya ujasusi kujibu hatua ya Bunge la Uturuki kupitisha azimio la serikali la kutuma askari nchini Libya.

Rais Sissi tayari amejadili suala hilo na marais wa Marekani, Urusi, Ufaransa na Kansela wa Ujerumani, ambao aliwapigia simu. Mazungumzo ambayo yalijikita kuhusu "athari ambayo inaweza kusababishwa na hatua ya nchi za kigeni kuingilia kijeshi Libya".

Rais wa Misri amesema Misri inaunga mkono suluhisho la "kisiasa" katika mzozo wa Libya, huku akibaini kwamba anaunga mkono vikosi vya Marshal Khalifa Haftar. Kufuatia shambulizi la hivi karibuni la Marshal Khalifa Haftar dhidi ya majeshi ya Tripoli Magharibi mwa nchi, kwenye mpaka wa Misri unaoendelea hadi Mashariki mwa Libya, kwenye umbali wa kilomita zaidi ya elfu moja , kwa sasa ni eneo ambalo liko salama.

Kwa upande wa serikali ya Cairo, inasema hatua ya Uturuki kutuma askari wake nchini Libya itapelekea wapiganaji wa kijihadi kutoka Syria kuingia kirahisi nchini Libya, na Misri kuwa hatarini.