LIBYA-UTURUKI-USALAMA

Askari wa Uturuki kuanza kupelekwa nchini Libya

Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan ametangaza kwamba wanajeshi wa Uturuki wameanza kupelekwa nchini Libya (picha ya kumbukumbu)
Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan ametangaza kwamba wanajeshi wa Uturuki wameanza kupelekwa nchini Libya (picha ya kumbukumbu) © Adem ALTAN / AFP

Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan ametangaza Jumapili jioni kuwa zoezi la kupeleka askari wa Uturuki nchini Libya limeanza. Siku ya Alhamisi wiki iliyopita Bunge la Uturuki lilipitisha azimio la serikali la kutuma askari wa nchi hiyo nchini Libya kusaidai serikali ya umoja wa kitaifa ya Tripoli. 

Matangazo ya kibiashara

Recep Tayyip Erdogan, ambaye hadi sasa amekuwa amejizuia kutoa maelezo yoyote ya kiutendaji kuhusu mpango wake wa kupeleka wanajeshi wa Uturuki nchini Libya, amesema kuwa zoezi hilo la kutuma askari nchini Libya linatarajiwa kuanza - bila hata hivyo kusema lini litaanza.

Kauli hiyo aliitoa wakati wa mahojiano kwenye runinga ya CNN Türk.

"Ujumbe wa askari wetu ni kuratibu. Na hilo ndilo wanalolifanya hivi sasa, kwenye kituo kimoja cha kijeshi. Mmoja wa maafisa wetu wa ngazi ya juu katika jeshi ataongoza kituo hiki cha kijeshi ... "

Akihojiwa kuhusu tarehe ya kupelekwa askari hao, rais wa Uturuki amejibu kuwa askari "wameanza kupelekwa kwa makundi."

"Pia tutakuwa na timu zingine huko kama vikosi vya kupambana, lakini askari wetu hawatakuwa katika vikosi hivyo, " amebaini.

Recep Tayyip Erdogan hakutoa maelezo zaidi kuhusu "vikosi hivi vya kupambana". Lakini katika wiki za hivi karibuni, kumekuwa na habari kuhusu kuwepo kwa wapiganaji wa Syria nchini Libya ambao wamewasili kutoka Uturuki kusaidia serikali ya umoja wa kitaifa.

Katika taarifa yake, balozi ya Marekani jijiniTripoli imelaani suala la "raia wa kigeni kuingilia kijeshi" Libya, ikitoa mfano na kutaja "kuwasili nchini Libya kwa wapiganaji wa Syria wanaoungwa mkono na Uturuki".