COTE D'IVOIRE-SIASA-USALAMA

Cote d'Ivoire: Ouattara apanga kufanya marekebisho ya Katiba kabla ya uchaguzi wa urais

Alassane Ouattara wakati wa kipindi cha Le Débat Africain kwenye RFI Desemba 3, 2019.
Alassane Ouattara wakati wa kipindi cha Le Débat Africain kwenye RFI Desemba 3, 2019. RFI

Rais wa Cote d'Ivoire Alassane Ouattara ametangaza kwamba anatarajia kufanyia marekebisho Katiba ya nchi hiyo kabla ya uchaguzi wa urais wa Oktoba, ambao unaonekana kama kipimo kwa usalama wa nchi.

Matangazo ya kibiashara

Mvutano uliibuka ghafla katika wiki za hivi karibuni kati ya Ouattara na wapinzani wake wa kisiasa, na kuongeza hofu ya kuongezeka kwa vurugumiezi tisa kabla ya uchaguzi nchini Cote d'Ivoire.

Machafuko ya baada ya uchaguzi wa mwaka 2010-2011 uligharimu maisha ya zaidi ya watu 3,000.

Akiongea mbele wanadiplomasia wa kigeni, Alassane Ouattara, ambaye bado hajatangaza nia yake ya kuwania au la katika uchaguzi wa mwezi Oktoba, amesema marekebisho yaliyopendekezwa yanalenga kuifanya katiba "iwe sawa", bila hata hivyo kutoa maelezo zaidi.

"Nataka kubainisha kwamba huu sio ujanja wa kumtenga yeyote katika uchaguzi huu," Ouattara amesema ili kuwahakikishia wapinzani ambao wana hofu kwamba kuna uwezekano aweke ukomo wa umri kwa wagombea wa urais , na hivyo kuwatenga wapinzani wake wakuu, ambao ni marais wa zamani Laurent Gbagbo na Henri Konan Bédié.

Marekebisho ya Katiba yanapaswa kupitishwa na bunge, linalodhibitiwa na washirika wa Ouattara.