LIBYA-EU-UTURUKI-URUSI-USALAMA

Mgogoro wa Libya: Nchi kadhaa zaungana na Walibya kutafutia suluhu mgogoro unaowakabili

Kiongozi wa Serikali ya umoja wa kitaifa ya Libya, Fayez el-Sarraj (kushoto) amepokelewa na Mkuu wa sera za mambo ya nje wa Ulaya Josep Borrell (katikati) na Charles Michel, rais wa Baraza la Ulaya, mnamo Januari 8, 2020.
Kiongozi wa Serikali ya umoja wa kitaifa ya Libya, Fayez el-Sarraj (kushoto) amepokelewa na Mkuu wa sera za mambo ya nje wa Ulaya Josep Borrell (katikati) na Charles Michel, rais wa Baraza la Ulaya, mnamo Januari 8, 2020. © Francisco Seco / AP Pool / AFP

Viongozi mbalimbali wanaendelea kushawishi pande husika katika mgogoro wa Libya ili kutafutia suluhisho la kudumu katika vita vinavyoendelea nchini humo.

Matangazo ya kibiashara

Katika hafla ya mkutano huko Istanbul, marais wa Urusi na Uturuki wametoa wito Jumatano wiki hii kwa pande husika katika mgogoro nchini Libya kusitisha mapigano.

Wakati huo huo Umoja wa Ulaya umemuahidi Fayez el-Sarraj kiongozi wa Serikali ya Libya inayotambuliwa na jumuiya kimataifa, kuimarisha juhudi nazozifanya kwa lengo la kupata suluhisho la amani.

Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan na mwenzake wa Urusi Valdimir Putine wote wametaka vita vivavyoendelea Libya kukoma mara moja. Wamependekeza mapigano hayo kusitishwa kuanzia Januari 12 saa sita usiku.

Kauli hii imewashangaza wengi wakati Uturuki inatetea Serikali ya umoja wa kitaifa, huku Urusi ikiunga mkono mbabe wa kivita mashariki mwa nchi hiyo Marshal Khalifa Haftar.

Katika tamko lao la pamoja, marais wa Uturuki na Urusi pia walielezea kuunga mkono kufanyika kwa mkutano wa kimataifa mwezi Januari jijini Berlin, mkutano ambao utawezesha kuzindua tena mchakato wa kisiasa chini mwamvuli wa Umoja wa Mataifa.

Libya inatawaliwa na serikali mbili za mashariki na magharibi na kila moja ikitegemea wanamgambo wa makundi tofauti. Serikali ya mashariki inaungwa mkono na Umoja wa Falme za Kiarabu na Misri pamoja na Ufaransa na Urusi huku ya Magharibi inayotambuliwa na Umoja wa Mataifa ikiwa inapata msaada kutoka Uturuki, Qatar na Italia.