NIGER-USALAMA

Kambi ya jeshi yashambuliwa Niger, askari wasiopungua 25 wauawa

Wanajeshi wa Niger wakipiga doria (picha ya kumbukumbu).
Wanajeshi wa Niger wakipiga doria (picha ya kumbukumbu). © ISSOUF SANOGO / AFP

Watu wenye silaha wanaoshukiwa kuwa wanamgambo wa kijihadi wameua wanajeshi 25 Alhamisi wiki hii na kujeruhi wengine sita katika shambulio dhidi ya kambi ya jeshi la Niger, magharibi mwa nchi, karibu na mpaka na Mali, serikali imebaini katika taarifa.

Matangazo ya kibiashara

Washambuliaji sitini na tatu pia wameuawa wakati wa mapigano hayo, ambayo yalitokea katika mji wa Chinagodrar, karibu kilomita 200 kaskazini mwa mji mkuu wa Niger, Niamey, mamlaka imesema.

Shambulio hilo ambalo halijadaiwa na kundi lolote, linajumuishwa katika machafuko makubwa yanayoendelea kuongezeka kutokana na makundi yenye mafungamano na Al Qaeda na kundi la Islamic State (IS), ambayo yanajaribu kushinikiza jeshi la Niger kuondoka kwenye maeneo ya mpakani na Mali.

Mwezi uliopita, shambulio kwenye kambi nyingine ya jeshi, kilomita 150 magharibi mwa Chinagodrar, liliua askari 71 wa Niger.