UFARANSA-SAHEL-USALAMA

Mkutano wa kilele wa Pau: Ufaransa yataka 'ufafanuzi' kuhusu uwepo wa askari wake Sahel

Askari wa Ufaransa kutoka kikosi cha Ufaransa cha Barkhane huko Tin Hama, Mali, Oktoba 2017.
Askari wa Ufaransa kutoka kikosi cha Ufaransa cha Barkhane huko Tin Hama, Mali, Oktoba 2017. © REUTERS/Benoit Tessier/File Photo

Mkutano wa kilele kuhusu hali katika ukanda wa Sahel unafanyika leo Jumatatu katika mji wa Pau, wiki tano baada ya mwaliko wa Emmanuel Macron kwa wenzake wa ukanda wa Sahel.

Matangazo ya kibiashara

Mkutano huu uliahirishwa kwa sababu ya shambulio dhidi ya kambi ya jeshi ya Inatès Desemba 11, 2019.

Baada ya vifo vya askari 13 wa Ufaransa nchini Mali, mwishoni mwa mwezi Novemba, ikulu ya Élysée inasubiri kutoka kwa marais hao wa ukanda wa Sahel "ufafanuzi" zaidi kuhusu uwepo wa askari wa Ufaransa katika ukanda huo, wakati ambapo baadhi ya raia kutoka Mali na Burkina Faso wameendelea kuonyesha msimamo wao wa kupinga uwepo wa askari wa Ufaransa katika nchini zao.

Rais wa Ufaransa anaonekana kukerwa na msimamo huu wa baadhi ya raia wa nchini hizi mbili kupinga uwepo wa vikosi vya Ufaransa katika Ukanda wa Sahel, baada ya kuandika nyaraka kwa marais wao kuhusu vikosi hivyo vya Ufaransa Desemba 4, 2019.

"Nasubiri ufafanuzi zaidi kutoka kwao na kurasimisha ombi lao kwa Ufaransa na jamii ya kimataifa. Wanahitaji vikosi vyetu huko? Je! Wanatuhitaji? Ninataka majibu yaliyo wazi na ya kweli kuhusu maswali haya, " amesema rais wa Ufaransa.