MALI-USALAMA

Mali: Kumi na nne wauawa katika kijiji cha Sinda

Kijiji cha Sinda kinapatikana kwenye umbali wa kilomita 12 kutoka mji wa Douentza, katikati mwa Mali (picha ya kumbukumbu)
Kijiji cha Sinda kinapatikana kwenye umbali wa kilomita 12 kutoka mji wa Douentza, katikati mwa Mali (picha ya kumbukumbu) © CC BY 2.0/wikimedia Commons/Makadaka

Raia 14 waliuawa usiku wa Jumatano kuamkia Alhamisi wiki hii katika kijiji Sinda, karibu na Douentza, katika mkoa wa Mopti, katikati mwa Mali, kwa mujibu wa vyanzo kutoka eneo hilo.

Matangazo ya kibiashara

Kulingana na ripoti ya Tume ya Haki za Binadamu na Ulinzi ya Umoja wa Mataifa, ambayo AFP ilipata kopi, "watu 14 waliuawa, 2 walijeruhiwa, vibanda kadhaa viliteketezwa kwa moto wakati wa shambulio dhidi ya kijiji cha Sinda, karibu na Douentza, katika mkoa wa Mopti ”.

"Ilipofika saa 12:30 asubuhi Januari 16, watu wenye silaha waliovalia mavazi ya wawindaji wa jadi (Dozos) ambao walikuwa kwenye pikipiki walivamia kijiji cha Sinda, kinachokaliwa na idadi kubwa ya watu kutoka jamii ya Fulani na kuanza kuwafyatulia risase wakazi wa kijiji hicho, wakitumia bunduki za kuwinda na kuchoma moto nyumba kadha ", inasema ripoti hiyo.

Hapo awali, chanzo cha usalama nchini Mali kiliripoti vifo vya raia kumi na tano.

"Wengine walijinjwa wakiwa usingizini , wengine baada ya kukamatwa na watu hao waliojifananisha na wawindaji wa jadi wanaojulikana kama" Dozos " au huenda walijifananisha kama wao," mbunge moja kutoka Douentza ambaye hakutaka jina lake litajwe kwa sababu za usalama, amesema.

Wahanga walizikwa Alhamisi wiki hii na wakaazi wa kijiji hicho, mwalimu mmoja kutoka Sinda ameliambia shirika la habari la AFP.

Tangu kuonekana mwaka 2015 kundi la mhubiri mwenye itikadi kali Amadou Koufa, katikati mwa Mali, akiajiri hasa wapiganaji kutoka jamii ya Fulani, ambao asili yao ni wafugaji, makabiliano ymeongezeka kati ya jamii hii na kabila za Bambara na Dogon, ambao wanajihusisha hasa na kilimo, waliounda "kundi lao la kujilinda na kujihami" .