LIBYA-BERLIN-USALAMA

Mkutano wa Berlin kuhusu mchakato wa amani Libya waandaliwa

Waziri wa Mambo ya nje wa Ujerumani Heiko Maas (kushoto) alikutana na Marshal Khalifa Haftar (kulia) Alhamisi hii, Januari 16.
Waziri wa Mambo ya nje wa Ujerumani Heiko Maas (kushoto) alikutana na Marshal Khalifa Haftar (kulia) Alhamisi hii, Januari 16. © uswaertiges Amt/Xander Heinl/photothek.de/Handout via REUTERS

Mkutano wa kimataifa kuhusu Libya utafanyika jijini Berlin, nchini Ujerumani chini ya mwamvuli wa Umoja wa Mataifa, Jumapili hii, Januari 19. Mkutano huo unalenga kufufua mchakato wa amani kwa nchi hiyo inayoendelea kukumbwa na mgogoro kwa miaka kadhaa.

Matangazo ya kibiashara

Kiongozi wa serikali ya umoja wa kitaifa nchini Libya, Fayez el-Sarraj, na mbabe wa kivita, Mashariki mwa Libya, Marshal Khalifa Haftar, wote wawili watarajiwa kushiriki mkutano huo nchini Ujerumani.

Fayez el-Sarraj alithibitisha Alhamisi hii wiki hii kwamba yuko tayari kushiriki mkutano huo. Na Khalifa Haftar amekubali kushiriki, kwa mujibu wa waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani, aliyekutana naye jijini Benghazi, nchini Libya. Ameongeza kuwa yuko tayari kuheshimu makubaliano ya kusitisha mapigano.

Makubaliano ya kusitisha mapigano yalianza kutetekelezwa Jumapili Januari 12, karibu na Tripoli, miezi tisa baada ya vikosi vya Marshal Khalifa Haftar kuanzisha mashambulizi kuelekea mji mkuu wa Libya, Tripoli.

Mkutano huu, uliopangwa kufanyika Berlin siku ya Jumapili, utafanyika wiki moja baada ya ule uliofanyika jijini Moscow, uliyoandaliwa chini ya mwamvuli wa Urusi na Uturuki.